1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISLAMABAD: Musharraf sasa huru kugombea urais huku bado akiwa mkuu wa jeshi

28 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBLw

Malalamiko yaliyowasilishwa dhidi ya hatua ya jenerali Pervez Musharraf wa Pakistan, ya kutaka kugombea awamu ya pili ya kipindi cha miaka mitano cha urais katika uchaguzi wa Oktoba 6 yamekataliwa na mahakama ya Pakistan.

Jopo la majaji sita limeamua dhidi ya wenzao watatu kutupilia mbali malalamiko kumi yaliyowasilishwa na vyama vya upinzani, makundi ya kutetea haki za kiraia na watu binafsi.

Katika uamuzi wake jopo hilo limesema kuwa rais Musharraf ana haki ya kugombea kiti chake huku akiwa bado anashikilia cheo chake cha kijeshi.

Mawakili wa upinzani wamesema wanapanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa mahakama.

Mapema mwezi huu rais Musharraf alisema kwamba ataachia madaraka yake ya kijeshi iwapo atachaguliwa tena kuiongoza Pakistan.

Tume ya uchaguzi ya Pakistan imearifu kuwa wagombea 43 mpaka sasa wameonyesha nia ya kutaka kugombea kiti cha urais.