1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Biden ataka Israel kuhakikisha wanawalinda raia

Lilian Mtono
26 Oktoba 2023

Rais wa Marekani Joe Biden amesema jana kwamba Israel ilikuwa na haki ya kujibu shambulizi la Hamas la Oktoba 7, lakini akiitaka Israel kufanya kila linalowezekana kuwalinda raia.

https://p.dw.com/p/4Y2HS
Rais wa Marekani Joe Biden ameitolea wito Israel kuwalinda raia wa Gaza hata katika mazingira magumu wakati inapopambana na Hamas
Rais wa Marekani Joe Biden ameitolea wito Israel kuwalinda raia wa Gaza hata katika mazingira magumu wakati inapopambana na Hamas Picha: Jonathan Ernst/AFP

Kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Washington, rais Joe Biden amelishutumu kundi la Hamas linalotawala Gaza kwa kujificha nyuma ya raia wa Palestina wakati Israel inaposhambulia eneo hilo lililozingirwa, lakini akisisitiza kwamba Israel italazimika kufuata sheria za vita.

Soma piaMamia wahofiwa kuuawa kwenye shambulizi la hospitali Gaza

Biden alikuwa akizungumza na waandishi wa habari sambamba na waziri mkuu wa Australia Anthony Albanese anayezuru Washington. Amesisitiza Israel inatakiwa kufanya kila linalowezekana hata katika mazingira magumu yaliyopo kuhakikisha raia wanakuwa salama.

Moshi ukifuka katika eneo la Ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel Jumatatu, Oktoba 23, 2023
Moshi ukifuka katika eneo la Ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel Jumatatu, Oktoba 23, 2023Picha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Lakini kwa upande mwingine, Biden amesema mashambulizi ya walowezi wa Israel dhidi ya Wapalestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi ni lazima yakomeshwe sasa, akisema hiyo ni kama kumwaga mafuta ya dizeli kwenye moto na kuongeza kuwa si sawa kuwashambulia Wapalestina kwenye maeneo wanayostahili kuwepo.

Ni kutokana na hayo yote, Biden akasema ni lazima kuwepo na namna ya kupata amani ambayo ni pamoja na suluhu ya mataifa mawili ya Israel  na Palestina.

Hadi sasa zaidi ya Wapalestina 6,500 wameuawa, wengi wao wakiwa ni raia katika mashambulizi ya kisasi ya Israel dhidi ya kundi la Hamas, hii ikiwa ni kulingana na wizara ya afya ya Gaza. Biden hata hivyo anatilia mashaka idadi hiyo.

Taarifa za awali zimesema shule moja inayowahifadhi watu 4,600 na inayoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi huko Palestina, UNRWA, iliathirika, baada ya jengo moja lililo karibu na shule hiyo kushambuliwa, limesema shirika hilo.

Soma pia:Mashirika ya kimataifa yaendelea kuonya juu ya hali tete inayounyemelea Ukanda wa gaza kutokana na mzingiro 

Rais wa ufaransa Emmanuel Macron akizungumza sambamba na rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi ambao kwa pamoja wameonya juu ya mashambulizi ya ardhini ya jeshi la Israel
Rais wa ufaransa Emmanuel Macron akizungumza sambamba na rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi ambao kwa pamoja wameonya juu ya mashambulizi ya ardhini ya jeshi la Israel Picha: Christophe Ena/AP/dpa/picture alliance

Huku hayo yakijiri, jana jioni, waziri mkuu Benjamin Netanyahu amesema kwenye hotuba iliyorushwa kwenye televisheni kwamba Israel inajiandaa kwa mashambulizi ya ardhini, ingawa hakufafanua kwa kina, zaidi ya kusema tu kwamba maamuzi juu ya muda wa uvamizi huo yatafikiwa kwenye makubaliano ya baraza maalumu la vita la serikali na kurudia kuwaomba raia walioko Gaza kuondoka.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron lakini ameipinga operesheni hiyo ya ardhini akisema litakuwa ni kosa na kuongeza kuwa yatawatia raia kwenye hatari kubwa. Alikuwa akizungumza na rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sissi, ambaye pia ameonya dhidi ya mashambulizi hayo.

Netanyahu aidha ameahidi uchunguzi wa kina ili kung'amua ombwe la kiusalama lililosababisha mashambulizi ya Oktoba 7 na kusema kila muhusika atalazimika kujibu, ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe. Lakini amesema, hilo litafanyika baadae.

Na huko New York, Urusi na China zimepigia kura ya turufu muswada wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na vita vya Israel dhidi ya Hamas. Muswada huo ulioandaliwa na Marekani unalenga kushughulikia mzozo wa kibinaadamu unaozidi kuongezeka katika Ukanda wa Gaza na kutoa mwito wa kusitishwa kwa mapigano ili kuruhusu misaada kuingia Gaza.

Umoja wa Falme za Kiarabu pia ulipinga muswada huo, huku wanachama wengine 10 wakiuunga mkono. Wanachama wawili hawakupiga kura.