1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel inawazika kwa heshima za kijeshi wanajeshi wake wawili waliokabidhiwa jana chini ya mpango wa kubadilishana wafungwa.

Saumu Mwasimba17 Julai 2008

Huzuni imetanda Kote Israel wakati walebanon wakisherekea kuachiliwa huru wapiganaji wa Hezbollah

https://p.dw.com/p/Ee4j
Maelfu ya walebanon wakisherehekea kuchiliwa huru wapiganaji wao na Israel''Picha: AP

Maelfu ya waisreali wamekusanyika kwenye mazishi ya Ehud Goldwasser yanayofanyika kwenye makaburi ya kijeshi katika mji alikozaliwa wa Nahriya kaskazini mwa Israel huku maelfu ya watu wakitarajiwa kuhudhuria baadae leo hii mazishi ya Eldad Regev yatakayofanyika kwenye makaburi ya kijeshi ya mji wa Haifa.

Majonzi yametanda kwenye mazishi ya Goldwaaser mwanajeshi aliyezuiliwa mateka kwa muda wa miaka miwli na kundi la Hezbollah na hatiae kurudishwa kwao hapo jana akiwa ni maiti.

Maelfu ya watu wamehudhuria mazishi yake leo hii akiwemo mjane wake Karnit wazazi wake na marafiki pamoja na wanasiasa.

Jeneza lililokuwa na maiti ya mwanajeshi huyo lilifunikwa bendera ya Israel na kubebwa hadi makaburini na wanajeshi wenzake wa kikosi maalum kilichoko katika eneo la Golan huku viongozi wa dini ya kiyahudi wa kijeshi wakiongoza ibada maalum ya mazishi.

Waziri wa Ulinzi wa Israel na mkuu wa zamani wa jeshi Ehud Barak pia alikuweko katika mazishi hayo.Alikuwa mnyonge na mwenye huzuni nyingi wakati akitoa buriani kwa mwanajeshi huyo amesema na hapa nikimnukuu'' Tulitaka kukukaribisha tena pamoja na mwenzako Eldad Regev.Tulitaka kuwakumbatia na kuwaona mkitabasamu lakini tunawasindikiza leo hii machozi ya kitudondoka huku mioyo yetu ikiwa mizito.''Mwisho wa kumnuku waziri wa ulinzi wa Israel Ehud Barak.

Kwa upande mwingine Rais Shimon peres amesema wamejitoa muhanga ili kuhakikisha roho za wanajeshi wake wawili zinalazwa mahala pema na huo ndio wanaouita ushindi na kwa hilo Lebanon imejidhalilisha.Lakini pia amesema Israel ina majonzi makubwa kutokana na kuwapoteza wanajeshi wake hao.

Hali nchini Lebanon ni ya huzuni iliychanganyika na furaha wakati maiti za wapiganaji wake 200 zikipitishwa kwenye mji mkuu Beirut wakaazi wakirusha maua ya wardi na mchele kwenye majeneza ya maiti hizo.

Majeneza hayo yamefunikiwa bendera ya taifa la Lebanon na ile ya kundi la Hezbollah na kupambwa na mashada ya maua huku magari yaliyoyabeba majeneza yakiwa na mabango yaliyoandikwa mashujaa wa vita.

Lebanon imefurahishwa sana na hatua ya Israel ya kuwakabidhi wafungwa wake waliokufa na wale watano waliohai .Punde tu baada ya hapo jana kuachiliwa huru wapiganaji hao rais Michel Suleiman alisema ''Lebanon ina haki ya kupigania kwa njia yoyote ile ardhi zake zilizonyakuliwa''

Kiongozi wa kundi la Hezbollah Sayyed Haasn Nasrallah alionekana hadharani ghafla akiwakaribisha wafungwa watano waliokuwa katika jela za Israel mjini Beirut na kukitaja kitendo hicho cha ubadilishanaji wafungwa na Israeli kuwa ni ushindi wa Hezbollah na Lebanon kwa jumla.

Maswahiba wakubwa wa Hezbollah Iran pia imefurahia kuachiwa huru wafungwa hao . Iran imesema ni habari za kufurahisha ambazo zimetokana na mafanikio ya upinzani wa kiislamu wa kundi la Hezbollah na taifa la walebanon.Waziri wa mambo ya nje wa Iran Manoucher Mottaki amesema yote hayo ni kufuatia ujasiri wa muda mrefu wa walebanon na mataifa ya eneo hilo.