1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel kuanza kuwatimua wahamiaji wa Kiafrika

Saumu Mwasimba
5 Februari 2018

Israei yatoa ilani kwa maelfu ya wahamiaji wa kiafrika ikiwataka waondoke kufikia mwezi Machi. Maafisa wanasema kwamba endapo onyo hilo halitotekelezwa wahamiaji huenda wakajikuta wakikamatwa na kufungwa jela.

https://p.dw.com/p/2s8HC
Israel eritreische Flüchtlinge demonstrieren in Jerusalem
Wakimbizi wakiafrika walipoandamana Jerusalem 17.01.2018Picha: picture-alliance/dpa/I. Yefimovich

Israel imeanza kutoa onyo kwa maelfu ya wahamiaji wa kiafrika tangu hapo jana ikiwataka waondoke nchini humo kufikia mwezi Machi. Maafisa wanasema kwamba endapo onyo hilo halitotekelezwa wahamiaji huenda wakajikuta wakikamatwa na kufungwa jela.

Maafisa nchini Israeli wameshaanza hatua ya kugawa vikaratasi vya ilani kwa wahamiaji wa kiafrika kuanzia hapo jana wakitakiwa kufunganya virago kwa khiari na kuiaga nchi hiyo chini ya mpango maalum unaolenga kuwaondowa kiasi watu 38 elfu wanaoomba hifadhi katika taifa hilo la Mashariki ya Kati, amesema msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Israel.

Ilani hiyo inayotowa muda wa miezi miwili  kwa wahamiaji kuondoka inatajwa kwamba inatolewa kwa wanaume wasiokuwa na watoto. Serikali ya Israel inawataja waomba hifadhi walioko nchi humo  kuwa ni wahamiaji wanaotafuta maslahi ya kiuchumi ikiwaita kwamba ni watu waliojipenyeza nchini humo.

Hivi karibuni waziri mkuu Netanyahu alisikika akisema:

''Watu waliojipenyeza kinyume cha sheria nchini wana chaguo rahisi-ama kutoa ushirikiano na sisi na kuondoka kwa khiari,kwa heshima na kihalali au tutalazimika kutumia njia nyingi zilizoko kwenye uwezo wetu,na ambazo pia ziko kisheria.Nataraji kwamba wataamua kushirikiana nasi.''

Uganda Besuch des israelischen Ministerpräsidenten Netanjahu
Waziri mkuu Netanyahu akiwa Uganda na rais Museveni Julai 2016Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Wandera

Kwa mujibu wa mpango wa Israel wahamiaji watakaoamua kuchagua kuondoka kwa khiari watapewa dolla 3,500 pamoja na tiketi ya ndege  ya kwenda nchi nyingine ambayo haikutajwa. Wanawake ,watoto na kina baba wanaotegemewa na watoto wao hawaguswi katika mpango huo. Hata hivyo kuanzia mwezi Aprili kiwango cha dolla 3500 zinazotolewa kitapunguzwa taratibu na endapo kuna mhamiaji aliyeamua kubakia katika nchi  hiyo atakuwa katika uwezekano wa kufungwa jela.Wengi wa wakimbizi wanasema wanakhiari kufungwa kuliko kurudishwa barani Afrika. Uamuzi wa Isreal umekosolewa na mashirika mbali mbali ya kutetea haki za binadamu.

Tamara Newman, mkurugenzi wa mahusiano ya kimataifa katika kitengo maalum kinachowashughulikia wakimbizi na wahamiaji Israel anasema:

''Mpango wa Israel wa kuwaondoa waomba hifadhi 38,0000 kuwapeleka Rwanda  pasipo khiari yao ni kitu kisichokubalika kabisa katika nchi yenye demokrasia ambayo imetia saini makubaliano ya kimataifa kuhusu wakimbizi. Serikali inawaambia wahamiaji sasa kwamba wana njia mbili za kuchagua ama kupelekwa Rwanda au kutiwa jela kwa kipindi kisichojulikana. Hili sio chaguo la kweli.tafiti zote zimetuonesha kwamba wote waliopelekwa Rwanda maisha yao yamezidi kuwa hatarini''

Wengi wa watu wanaoomba hifadhi nchini Israel wanaokabiliwa na hali hiyo ya kuondolewa kwa nguvu ni raia wa Sudan na Eretrea. Kadhalika Uganda na Rwanda zinatajwa kwamba ni nchi ambazo wakimbizi hao huenda wakapelekwa ingawa nchi hizo zimekanusha kuwa ni vituo vya kuwapokea  wahamiaji watakaorudishwa Afrika kutoka Israel.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/afpe

Mhariri: Gakuba, Daniel