1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaashiria kutoshirikiana na Biden sera ya Iran

Amina Mjahid
16 Februari 2021

Israel imeondoa uwezekano wa kushirikiana kimkakati na serikali ya rais wa Marekani Joe Biden katika suala la mpango wa nyuklia wa Iran, ikihimiza uwepo wa vikwazo vikali na vitisho vya kijeshi dhidi ya adui yake Iran. 

https://p.dw.com/p/3pRZf
Jerusalem | Benjamin Netanyahu, Israel Katz und Gilad Erdan im Parlament
Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Scheiner

Matamshi hayo ya mjumbe wa Israel nchini Marekani Gilad Erdan, yamekuja wakati muhimu kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anaewania kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa mwezi ujao. Balozi Erdan amerejelea na kuonesha msimamo mkali wa Israel dhidi ya Iran akisema hakutokuwa na mawasiliano ya aina yoyote na rais Biden kuhusiana na mpango wa nyuklia wa Iran.

"Hatutaki kuwa sehemu ya mchakato huo iwapo utawala mpya wa Marekani utarejea kuyatambua makubaliano ya nyuklia ya Iran. Marekani ikifanya hivyo, itakuwa imejishusha hadhi na kujipotezea heshima duniani," alisema balozi Erdan.   

Rais Biden alisema ana mpango wa kuirejesha Marekani katika makubaliano hayo ya nyuklia yaliotiwa saini mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa sita yalio na nguvu duniani. Rais wa zamani Donald Trump aliiondoa Marekani katika makubaliano hayo na kuiwekea Iran vikwazo vikali vya kiuchumi. Lakini kwa sasa serikali ya rais mpya wa taifa hilo Joe Biden imesema inataka kuzungumza na washirika wake wa Mashariki ya Kati juu ya nia yake hiyo.

Israel Gilad Erdan
Mjumbe wa Israel nchini Marekani Gilad Erdan Picha: Getty Images/AFP/A. Gharabli

Wasaidizi wa Netanyahu wamekuwa wakihoji faraghani iwapo kushirikiana na wenzao wa Marekani kunaweza kuigeukia  Israel, kwa kuashiria isivyo kweli, ridhaa yake kwa makubaliano yoyote mapya ambayo bado inapinga. 

Israel haikuwa sehemu ya mpango wa nyuklia wa mwaka 2015. Lakini ina watetezi walio na nguvu ndani ya bunge la Marekani, na kitisho cha Netanyahu cha kuchukua hatua za upande mmoja za kijeshi dhidi ya Iran, iwapo atahisi diplomasia imeshindwa, ni sehemu ya mikakati ya kuonesha nguvu yake.

Balozi Erdan alisema wanadhani kwamba vikwazo vikali sambamba na kitisho cha kweli cha kijeshi - ambavyo Iran inahofia - ndiyo vinaweza kuileta Iran kwenye mazungumzo ya kweli na mataifa ya magharibi, hatua ambayo inaweza kuzaa makubaliano yenye uwezo wa kweli wa kuizuwia kutengeneza silaha za nyuklia huko mbeleni.