1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yakumbuka mauaji ya halaiki ya Wayahudi milioni sita

Charo Josephat21 Aprili 2009

Rais Shimon Peres asema chuki dhidi ya Wayahudi bado ingalipo

https://p.dw.com/p/HbDc
Rais wa Israel Shimon PeresPicha: AP

Sauti ya ving´ora imesababisha shughuli kusita nchini Israel mapema leo huku taifa hilo likiwakumbuka wayahudi milioni sita waliouwawa na manazi wa Ujerumani wakati wa vita vya pili vya dunia. Rais wa Israel Shimon Peres ameonya kwamba chuki dhidi ya wayahudi bado ingalipo, miaka 64 tangu kushindwa kwa utawala wa manazi na kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia.

Wakati wa dakika mbili za utulivu na kunyaa kimya kote nchini Israel hii leo, watu waliokuwa wakitembea barabrani walisimama, baadhi yao wakiinamisha vichwa vyao. Madereva wa magari nao pia wamesimamisha magari yao huku taifa hilo la kiyahudi likiikumbuka siku ya mauaji ya wayahudi, "Holocaust".

Hii leo kumbukumbuku za pamoja zinafanyika siku moja baada ya rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad, ambaye mara kwa mara ameyaeleza mauaji ya wayahudi kuwa hadithi, kuzusha hisia za kumkosoa wakati alipoieleza Israel kuwa utawala katili, kandamizi na wenye ubaguzi. Rais Ahmedinejad aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa dhidi ya ubaguzi unaofanyika mjini Geneva nchini Uswisi.

Israel ilianza kumbukumbu hizo machweo ya jua hapo jana kwa sherehe iliyofanyika katika ukumbi wa kumbukumbu wa Yad Vashem mjini Jerusalem, ambako manusura wa mauaji ya manazi waliwasha mishumaa sita kuwakumbuka wahanga wa mauji hayo.

Rais wa Israel, Shimon Peres, ameonya kwamba chuki dhidi ya wayahudi ingalipo, na kuukosoa mkutano dhidi ya ubaguzi unaoendelea mjini Geneva Uswisi. Kiongozi huyo pia ameukosoa Umoja wa Mataifa kwa kumruhusu rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, kuuhutubia mkutano huo.

Benjamin Netanjahu wird Außenminister Israels
Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: AP

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kwa upande wake ameapa kuwa kamwe hatoruhusu watu wanaokana kutokea kwa mauaji ya halaiki ya wayahudi, kufanya tena mauaji mengine ya wayahudi. Aidha Netanyahu amesema ni jukumu kubwa la taifa la Israel kuwalinda raia wake dhidi ya mauaji mengine.

Netanyahau ameukosoa mkutano wa Umoja wa Mataifa dhidi ya ubaguzi unaoendelea mjini Geneva, Uswisi. Amemkosoa vikali rais wa Uswiwi, Hans-Rudolf Merz, kwa kukutana na rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, ambaye Netanyahu anamueleza kuwa mtu anayekana kutokea kwa mauaji ya "holocaust".

Umoja wa Mataifa umeweka Januari 27, siku ambapo kambi ya mateso ya Auschwitz nchini Ujerumani ilikombolewa mnamo mwaka 1945, kuwa siku ya kimataifa ya kukumbuka mauaji ya wayahudi milioni sita. Lakini kitamaduni Israel hufanya kumbukumbu hiyo siku ya 27 ya mwezi wa kiyahudi wa Nissan, wiki moja kabla siku ya uhuru ili kuashiria kuzaliwa kwa taifa la kiyahudi kutoka kwa mavumbi ya mauaji ya holocaust.

Kama sehemu ya kumbukumbu hizo king´ora hulia nchini kote mwendo wa saa nne asubuhi na Waisraeli husimama wima wakiwa kimya kutoa heshima zao kwa wahanga wa mauaji ya manazi. Majina ya wahanga, au majina yanayojulikana, yatasomwa katika bunge la Israel, Knesset na kwenye ukumbi wa kumbukumbu wa Yad Vashem.

Kwa mujibu wa takwimu za kabla na baada ya vita vya pili vya dunia, thuluthi mbili kati ya wayahudi milioni tisa waliokuwa wakiishi barani Ulaya waliangamia mikononi mwa manazi na washirika wao. Milioni 1.5 kati yao walikuwa watoto. Kauli mbiu ya makumbusho ya mwaka huu ni watoto waliouwawa wakati wa mauaji hayo.

Mwanishi: Josephat Charo/DPAE

Mhariri: Abdul-Rahman