1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yapuuza mbinyo ya kimataifa na kuratibisha ujenzi, Jerusalem

24 Machi 2010

Wapalestina waendelea kukerwa, viongozi wa Kiarabu kukutana mwishoni mwa juma nchini Libya.

https://p.dw.com/p/Mb34
Netanyahu akihutubia kundi la ushawishi mkubwa wa Wayahudi, Marekani jumatatu wiki hii.Picha: AP

Mfanyakazi katika baraza la mji wa Jerusalem amesema mpango wa kujenga makaazi ya Walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ya Wapalestina walikofurushwa mwaka jana, umeratibishwa, jambo ambalo linawakera zaidi Wapalestina na kutishia mikakati ya kuleta amani inayoongozwa na magharibi.

Haya yanajiri chini ya saa ishirini na nne tangu waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kukutana kwa mazungumzo ya faragha na rais Barack Obama wa Marekani. Siku ya Jumatatu wiki hii, akihutubia kikao cha washawishi wakuu wa Kiyahudi nchini Marekani alisema Jerusalem ipo nchini mwao na ujenzi utaendelea kama Israel inavyopenda.

Katika tukio lisilo la kawaida, Saudi Arabia imelalamika kwa nchi zenye ushawishi zinazoendeleza mikakati ya amani mashariki ya kati, kufafanua kiburi cha Israel na sera zake zinazokiuka matarajio ya kimataifa.

Palästinensischer Präsident Abbas mit Saeb Erekat in Kairo
Msemaji, Bw. Erekat (kushoto) na rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas.Picha: picture alliance/dpa

Mpatanishi wa Palestina, Saeb Erekat anasema njama ya Israel ni kuwaondoa kwa nguvu Wapalestina mashariki mwa Jerusalem na kusambaratisha mchakato wowote wa mazungumzo ya amani.

Erekat alisema Israel inajitumbukiza katika shimo na itawajibika kujiondoa ikiwa inachukulia suala la amani kwa uzito.

Diwani wa Jerusalem, Elisha Peleg alisema katika mahojiano na stesheni ya redio ya kijeshi kwamba mipango ya ujenzi iliithinishwa kitambo na wataendelea kujenga makaazi ya walowezi mashariki mwa Jerusalem.

Hillary Rodham Clinton vor dem AIPAC
Bi Clinton, waziri wa mambo ya nje wa Marekani. Asisitiza ujenzi wa Israel unatishia amani.Picha: AP

Kwa upande wa Marekani Waziri wake wa mambo ya nje, Bi Hillary Clinton alisema hivi karibuni kwamba ujenzi huo unaleta hofu zaidi.

Katika taarifa inayoambatana na siasa mashariki ya kati, jeshi la Israel limeanzisha uchunguzi dhidi ya wanajeshi wake wawili wanaotuhumiwa kwa kuwaua kwa kufyatua risasi, wavulana wawili wa Kipalestina.

Israelische Soldaten patrouillieren das Gebiet entlang der Grenze zwischen Israel und dem Gaza-Streifen
Wanajeshi wa Israel wapiga doria mpakani mwa Israel na ukanda wa Gaza.Picha: AP

Mmoja wa washukiwa hao aliiambaia redio ya kijeshi kwamba wanatumiwa tu kuonyesha kwamba Israel inawajibika hasa kutokana na mbinyo ya kimataifa.

Wakati huo huo mpango wa Palestina wa kutaka kulipa jina bustani kutokana na Dalal Mughrabi, aliyekuwa mwanaharakati aliyeuawa wa Kipalestina umepingwa na Israel.

Kundi la Hamas pia limejitokeza katika mzozo huo na limetoa amri ya kunyongwa kwa wasaliti wa Kipalestina wanaoshirikiana na Israel.

Kwa upande mwengine viongozi wa nchi za Kiarabu watakutana nchini Libya katika mji kwenye ufuo wa Medditerranean wa Sirte kuanzia jumamosi wiki hii kupanga mikakati ya msimamo wa pamoja wa kukabiliana na Israel.

Mwandishi: Peter Moss /Reuters/AFP/AP/DPA

Mhariri: Abdul-Rahman Mohammed