1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yasema Libya haifai kuwa katika baraza la usalama

31 Januari 2008
https://p.dw.com/p/D05a

Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Dan Gillerman, ameishutumu Libya kwa kuendelea kukiri inaunga mkono ugaidi.

Aidha kiongozi huyo amependekeza kuwa Libya haifai kuwa na kiti katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Baada ya miongo ya kutengwa kama mpinzani wa nchi za magharibi Libya ilichaguliwa kuwa mwanachama wa baraza la usalama mwaka jana baada ya Marekani kufutilia mbali msimamo wake wa kuipinga.

Libya imekuwa rais wa baraza la usalama kwa mwezi huu wa Januari.

Wakati wa mjadala kuhusu Mashariki ya Kati, balozi wa Libya katika Umoja wa Mataifa, Gadalla Ettalhi, alimkasirisha mwenzake wa Israel kwa kulikosoa taifa hilo la kiyahudi kwa mauaji ya kikabila na ukiukaji wa mara kwa mara wa haki za binadamu katika maeneo ya wapalestina.

Akijibu balozi wa Israel alisema ipo haja ya kuzingatia michango ya mataifa katika kulinda amani ya dunia kabla kuyachaguliwa kuwa wanachama wa baraza la usalama.