1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yatikiswa na wimbi la mauaji

30 Machi 2022

Waziri Mkuu wa Israel Naftali Bennett amesema nchi hiyo inakabiliwa na wimbi la mauaji yanayochochewa na ugaidi baada ya kutokea shambulizi jingine ambalo limewauwa watu watano nje kidogo ya mji wa Tel Aviv.

https://p.dw.com/p/49DkT
Israel | Anschlag in Bnei Brak bei Tel Aviv
Picha: Ilia Yefimovich/dpa/picture alliance

Hamkani imetanda nchini Israel baada ya kutokea mashambulizi mfululizo tangu wiki iliyopita ambayo kwa jumla hadi sasa yamesababisha vifo vya watu 11 ukiondoa washambuliaji waliouwawa.

Hapo jana mtu mwenye bunduki ya rashasha aliwashambulia watu kwenye kitongoji cha Bnei Brak nje kidogo ya mji wa Tel Aviv. Watu watano akiwemo afisa mmoja wa polisi waliuwawa kwenye mkasa huo.

Polisi ya Israel  imesema mshambuliaji alikuwa kijana wa kipalestina mwenye umri wa miaka 27.  Aliingia kwenye wilaya ya Bnei Brak kwa pikipiki akitokea Ukingo wa Magharibi.

Kwanza aliwafyetulia risasi na kuwauwa raia wawili wa Ukraine na baadae wengine wawili raia wa Israel na kisha akammiminia risasi polisi mmoja wakati vikosi vya usalama vilipofika kumkabili. Polisi ya Israel ilimuua mshambuliaji huyo kwenye uwanja wa mapambano.

Waziri Mkuu wa Israel asema hilo ni "wimbi la mauaji ya kigaidi"

Naftali Bennett
Waziri Mkuu wa Israel Naftali BennettPicha: Tsafrir Abayov/Pool/picture alliance

Akizungumzia tukio hilo waziri mkuu wa Israel Naftali Benett amesema nchi yake inakabiliwa na wimbi hatari la mauaji yanayonasibishwa na kile amekitaja kuwa "ugaidi kutoka makundi ya waarabu"

"Raia wa Israel hizi, hivi sasa tunapitia kipindi kigumu. Kila baada ya miaka kadhaa, taifa la Israel hukabiliwa na wimbi la ugaidi. Baada ya muda wa utulivu, sasa kumezuka uhalifu unaofanywa na wale wanaojaribu kutuangamiza, wale wanaotaka kutudhuru kwa gharama yoyote, wale ambao chuki yao kwa wayahudi, na taifa la Israel inawatia wendawazimu. Wale ambao wako tayari kufa almuradi sisi hatuishi kwa amani." amesema Bennett 

Baadae leo Bennett anatarajiwa kuongoza kikao cha maafisa wakuu wa usalama kutathmini hali hiyo na polisi imesema vikosi vyote nchini humo vimewekwa katika hali ya juu ya tahadhari.

Usiku wa kumkia leo vikosi vya Israel vilifanya operesheni kubwa kwenye Ukingo wa Magharibi vimewakamata wapalestina watano inaowashuku wanahusiaka na shambulizi la mjini Tel Aviv.

Abbas alaani mauaji lakini kundi la Hamas layasifu 

Shambuzili la jana ni tukio la tatu la  aina hiyo kutokea nchini Israel tangu wiki iliyopita.

Israel Hadera | Zwei tote nach Angriff
Polisi wa Israel wakizingira eneo la mkasa wa mauaji huko kwenye mji wa Hadera Picha: Gil Cohen-Magen/AFP

Siku ya Jumapili polisi wawili kwenye mji wa kaskazini wa Hadera waliuwawa na washambuliaji wenye bunduki. Washambuliaji hao wawili waliohusika kwenye kisa hicho nao pia waliuwawa na maafisa wa usalama.

Mkasa wa Hadera ulitanguliwa na mwingine wa wiki iliyopita ambapo mtu mmoja awalidunga kisu na kuwauwa raia wanne wa Israel huko kwenye mji wa kusini wa Beersheba.

Kuna wasiwasi mashambulizi ya aina hiyo huenda yataongezeka kuelekea mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Wimbi hilo la mashambulizi limelaaniwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. Kiongozi wa mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmoud Abbas naye pia ametoa taarifa ya nadra kulaani visa hivyo vya mauaji.

Hata hivyo kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza limeyasifu mashambulizi ya aina hiyo likisema ni jibu kwa "uhalifu wanaotendewa watu wao" wakiamaanisha wapalestina.