1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yawakumbuka wahanga wa Holocaust

Mohammed Khelef
24 Aprili 2017

Ving'ora vililizwa kwa muda wa dakika mbili nchini Israel kuwakumbuka Mayahudi milioni sita waliouawa na utawala wa Kinazi wa Ujerumani kwenye mauaji ya Holocaust barani Ulaya, huku miito dhidi ya chuki kwa jamii hiyo.

https://p.dw.com/p/2bp8d
Israel Yad Vashem Gedenken
Picha: picture-alliance/Newscom/A. Cohen

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, Rais wa nchi hiyo, Reuven Rivlin, wameungana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, na Kansela Christian Kern wa Austria kwenye mnara wa Kumbukumbu wa Yad Vashem mjini Tel Aviv mapema leo kuyakumbuka mauaji hayo ya kikatili.

Katika hotuba yake ya alfajiri, Netanyahu alirejelea madai yake ya kuongezeka kwa chuki dhidi ya Mayahudi ulimwenguni, huku akimsifia mshirika wake mkuu, Rais Donald Trump, kama "miale ya nuru", hasa kwa mashambulizi ya hivi karibuni ya makombora dhidi ya Syria kwa kile kilichoelezewa kama jibu la mashambulizi ya kemikali yaliyodaiwa kufanywa na utawala wa Rais Bashar al-Assad dhidi ya raia.

"Japokuwa tangu Vita vya Pili vya Dunia hakujakuwa na msiba mkubwa kama Holocaust, lakini kumekuwa na matukio kadhaa ambayo yametokea na dunia haikuzuwia uangamizaji wa watu. Biafra, Cambodia, Rwanda, Sudan na pia nchini Syria, na kwa hili licha ya giza pana, kuna namna fulani ya miale ya nuru. Mmoja wao umetokea hivi punde na ni jibu makini la Rais Trump dhidi ya mauaji ya watoto wa Syria kwa silaha za kemikali. Hatujitengi na machungu wanayowapata watu wa Syria."

Trump aapa kuendelea kuilinda Israel

Poeln Auschwitz March of the Living
Sehemu ya vijana 10,000 wa Kiyahudi walioshiriki kwenye "Maandamano ya Kuishi" kutoka Auschwitz hadi Birkenau, miji iliyokuwa na makambi makubwa kabisa ya kuwatesea na kuwaulia Mayahudi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.Picha: picture-alliance/PAP/A. Grygiel

Naye Rais Trump, ambaye katika siku za karibuni serikali yako imekuwa ikitoa kauli zenye utata kuhusiana na mauaji hayo, alilihutubia taifa usiku wa kuamkia leo na kuendeleza ahadi ya Marekani kusimama pamoja na Israel katika hali zote, akisema kuwa chuki dhidi ya jamii ya Kiyahudi ni lazima ishindwe, akiyaita mauaji ya Holocaust kama "sura mbaya sana kwenye historia ya mwanaadamu.

"Katika kuwakumbuka wale tuliowapoteza, tunaendelea kuthibitisha dhamira yetu ya kutopuuzia vitisho vya wakati wetu. Lazima tupambane na dharau na chuki ya Mayahudi popote pale zinapojitokeza. Lazima tuushinde ugaidi, na lazima tusipuuzie kitishok cha wale wanaozungumzia waziwazi juu ya kuiangamiza Israel. Hatuwezi kuruhusu jambo hilo hata kuwaziwa kwake. Naifahamike wazi kuwa Marekani iko pamoja na Israel kwa kila hali."

Nchini Poland, zaidi ya vijana 10,000 wa Kiyahudi kutoka Israel na duniani kote walikusanyika kushiriki kwenye mbio za kila mwaka za kilomita mbili ziitwazo "Maandamano ya Kuishi" kutoka Auschwitz hadi Birkenau, miji ambayo yalikuwa na makambi makubwa kabisa ya kuwatesea na kuwaulia Mayahudi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Ujumbe mkubwa wa kumbukumbu za mwaka huu za Holocaust ni elimu kwa vijana juu ya kile kilichotokezea, ambapo mawaziri 12 wa elimu watakutana nchini Israel kupanga mkakati wa kuendeleza historia ya mauaji hayo, baada ya manusura kumalizika. Hadi sasa kuna manusura 160,000 waliobakia nchini Israel pekee.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga