1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia yaingia katika mdororo wa kiuchumi

Sekione Kitojo
31 Januari 2019

Italia imetumbukia tena katika mdororo wa kiuchumi, ikiongeza wasi wasi juu ya uchumi wa nchi 19 za kanda ya sarafu ya euro na  uwezekano wa hali mbaya ya madeni katika masoko ya kanda hiyo.

https://p.dw.com/p/3CWJ7
Italien Haushalt 2019 | Giuseppe Conte und Giovanni Tria
Waziri mkuu Giuseppe Conte , kushoto, akishikana mkono na waziri wa fedha Giovanni Tria wakati wakihudhuria mjadala wa bajeti ya mwaka 2019Picha: picture-alliance/AP Photo/G. Lami

Wakati  huo  huo kasi ya  ustawi  wa uchumi  wa mataifa  ya  kanda  ya  sarafu  ya  euro  imepungua  sana  hadi asilimia  1.8 katika  mwaka  2018.

Italien Genua Hafen mit Container
bandari ya Italia ya Genua ikiwa na makontenaPicha: picture-alliance/Bildagentur-online/AGF

Data zinaonesha  kwamba  kupungua  kwa  mauzo  ya  nje  nchini Ujerumani  na  wasi  wasi  kuhusiana  na   kujitoa  kwa  Uingereza katika  Umoja  wa  Ulaya  maarufu  kama  Brexit  kumepunguza  kasi hiyo  kwa  kiasi  kikubwa. Uchumi  wa  Italia , ukiwa  ni  uchumi  wa tatu  mkubwa  katika  kanda  ya  sarafu  ya  euro , ulinywea kwa kiwango  cha  kipindi  cha  robo  mwaka  kwa  asilimia  0.2  katika robo  ya  nne  ya  mwaka  2018, limesema  shirika  la  takwimu  la taifa nchini  Italia.

Kufuatia  kuporomoka  kwa  asilimia  0.1 katika  vipindi  vya  miezi mitatu  ya  nyuma  hii  ina  maana  Italia  imo  kimsingi katika hali  ya mdororo  wa  kiuchumi, inayotafsirika  kuwa  ni  vipindi  viwili mfululizo  vya  kunywea  kwa  uchumi kiasi  ya  miaka  minne  baada ya  hali  hiyo  kutokea  mara  ya  mwisho.

Mdororo  wa  kiuchumi  nchini  Italia  ni  sababu  mojawapo kwanini kanda  hiyo  ya  euro ilipungua  kasi  katika  ukuaji  wake  wa  uchumi katika  mwaka  2018, pamoja  na  hali  ya  sintofahamu inayohusiana  na  Brexit, mzozo  wa  kiuchumi  kati  ya  China  na Marekani pamoja  na  viwango  vipya  vya  utoaji  wa  gesi  chafu kwa  magari.

Symbolbild Italien & die EU
Bendera ya Italia pamoja na bendera ya Umoja wa UlayaPicha: Getty Images/AFP/P. Huguen

Shirika la  takwimu

Licha  ya  kuwa  kanda  ya  euro  inafanya  vizuri  kuliko  katika nyakati  za  giza  za  mzozo  wa  madeni , ambao  ulitishia  kuvunjilia mbali  umoja  huo  wa  sarafu, bado  uchumi  wake  uko  nyuma  ya Marekani, ambayo ilitabiriwa  kukua  kwa  asilimia  3  katika  mwaka 2018. Kutokana  na  hayo , ukosefu  wa  ajira  katika  kanda  ya sarafu  ya  euro  ni  kiasi  ya  mara  mbili  ya  asilimia  4  ya Marekani  inayofikia  asilimia  7.9.

Uchumi  wa  kanda  ya  sarafu  ya  euro ulikuwa  kwa  jumla  ya asilimia  0.2  tu  katika  robo  ya  mwisho  ya  mwaka  2018, sawa kama  katika  robo  iliyopita  ya  mwaka, kwa  mujibu  wa  tarakimu za  awali  zilizotolewa   leo  na  shirika  la  takwimu  la  Eurostat.

Uchumi  huo umepanuka  kwa  asilimia  1.8  katika  mwaka  2018  kwa  jumla , ikiwa  ni kiwango  chake  dhaifu  kabisa  katika  muda  wa  miaka  minne. Hii ni  chini kuliko  ilivyotarajiwa  mwaka  mmoja  uliopita, wakati  kundi hilo  la  mataifa  lilipotarajiwa  kupunguza  kasi  ya  ukuaji  wa  uchumi kwa  kiasi  kidogo  kutoka   ukuaji  mkubwa  wa  mwaka  2017  wa asilimia  2.4.

Italien | Demonstranten fordern Strecke nach Lyon in Turin
Maandamano ya umma nchini Italia dhidi ya vuguvugu la Nyota tano , mwaka Novemba 10, 2018Picha: picture alliance / picture-alliance/dpa/NurPhoto/M. Ujetto

Uchumi  wa  Italia  umekuwa  chachu  ya  chanzo  cha  wasi  wasi katika  muda  wa  miezi  michache  iliyopita, kwa  sehemu  fulani ikiwa  ni  matokeo  ya msuguano wa serikali  mpya  ya  siasa  za kizalendo na  halmashauri  ya  Umoja  wa  ulaya  kuhusiana  na mipango  ya  bajeti  yake, hali  ambayo  imedhoofisha  imani  ya wafanyabiashara na  kushuhudia  viwango  vya  kukopa   katika masoko  ya  hisa   vya Italia vikiongezeka kwa  kiwango  cha  juu kabisa.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape

Mhariri: Idd Ismail  Ssessanga