1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jammeh afungia redio inayomkosoa

Sekione Kitojo
2 Januari 2017

Serikali ya Gambia imekifungia kituo maarufu cha redio binafsi kiitwacho Taranga FM katika wakati ambapo muda wa kuondoka madarakani kwa Rais Yahya Jammeh ukikaribia licha ya kuapa kuendelea kubakia.

https://p.dw.com/p/2V8Z7
Gambia Präsident Yahya Jammeh
Picha: Reuters/T. Gouegnon

Chama cha waandishi habari nchini humo kimeonya kwamba  kufungwa kwa kituo hicho cha redio kunaashiria mwanzo wa ukandamizaji dhidi ya vyombo vya habari vya watu binafsi, hasa vile ambavyo vinatoa nafasi ya mawazo yanayopingana na serikali.

Redio Taranga FM kinaonekana kuwa kinamkosoa Rais Jammeh, ambaye alishindwa uchaguzi Disemba a mpinzani wake, Adama Barrow, aliyesimama kwa niaba ya muungano wa upinzani. 

Awali, Jammeh alikuwa amekubali kushindwa na akampongeza Barrow, lakini wiki moja baadaye alilitangazia taifa hilo la Afrika Magharibi kwamba hakubaliani na matokeo ya uchaguzi, akidai kuwapo na mapungufu makubwa na chama chake kiliwasilisha pingamizi katika Mahakama ya Juu kutengua matokeo hayo.

Hatua hiyo ya Jammeh ililaaniwa ndani na nje ya nchi yake, huku Jumuiya ya Uchumi ya Afrika ya Magharibi (ECOWAS) ikiapa kumuondoa kwa nguvu kama atakataa kuondoka kwa hiyari baadaye mwezi huu.