1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Japan na Australia zaboresha mkataba wao wa usalama

22 Oktoba 2022

Japan na Australia zimetia saini leo mkataba mpya wa ushirikiano wa usalama unaohusu masuala ya kijeshi na ujasusi ili kukabiliana na tatizo la kuzorota kwa usalama na kuongezeka kwa uthubutu wa China.

https://p.dw.com/p/4IYJW
Japanischer Premierminister Kishida Fumio und australischer Premierminister Anthony Albanese
Picha: Richard Wright/imago images

Matokeo ya mkutano huo kati ya Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida na mwenzake wa Australia Anthony Albanese katika pwani ya magharibi ya mji wa Perth, ilikuwa uboreshaji wa Azimio la Pamoja la Ushirikiano wa Usalama, ambapo Mkataba wa kwanza ulitiwa saini mwaka 2007 wakati ushawishi wa China haukuwa wa kutia wasiwasi mkubwa.

Mkataba huo unatokana na makubaliano ambayo Kishida alisaini mwezi Januari na Waziri Mkuu wa wakati huo wa Australia Scott Morrison, na kukubaliana kuondoa vikwazo vya kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi katika nchi hizo.

Soma zaidi: Australia na Japan zaimarisha ushirikiano wao wa kijeshi kukabiliana na China

Maafikiano kama hayo ni ya kwanza ambayo Japan imesaini na nchi nyingine, mbali na Marekani. Chini makubaliano hayo, Japan imetangaza leo Jumamosi kuwa vikosi vyake vya ulinzi vitashiriki kwa mara ya kwanza katika mazoezi ya pamoja na Jeshi la Australia, kaskazini mwa nchi hiyo.

Infografik Karte Indo-Pazifischer Raum EN
Ramani ya Ukanda wa Hindi na pasifiki.

Katika muktadha wa makubaliano hayo, Albanese amewaambia waandishi wa habari kuwa huo ni uamuzi wa kihistoria na unatoa ishara kali na ya kimkakati kwa eneo hilo.

Makubaliano hayo yanahusu ushirikiano wa kijeshi, ujasusi, usalama wa mtandao, shughuli za uendeshaji wa teknolojia ya sayari, utekelezaji wa sheria, ulinzi wa vifaa na mawasiliano. Makubaliano hayo yanahusu pia ushirikiano katika "kupinga uchumi kandamizi na upotoshaji wa habari", vitisho ambavyo China inashutumiwa.

Mazingira magumu katika ukanda wa Hindi na Pasifiki

Nordkorea Raketentest Fumio Kishida
Waziri Mkuu wa Japan, Fumio KishidaPicha: Kyodo/REUTERS

Kishida amesema mfumo mpya wa ushirikiano umeandaliwa huku mazingira ya kimkakati yakizidi kuwa magumu, na kwamba hii itaonyesha mwelekeo wa ushirikiano wao wa kiusalama na ulinzi katika miaka 10 ijayo.

Mawaziri wakuu hao wawili wamebaini kuwa makubaliano hayo mapya yana lengo la kuiimarisha Japan na mikataba yake ya usalama pamoja na nchi za  Australia na Marekani ambazo zinasimamia amani na utulivu katika ukanda wa Hindi na Pasifiki.

Ziara ya Kishida kwa mkutano wa kilele kati ya nchi hizo mbili ni ya nne kukutana na Albanese tangu serikali ya kiongozi huyo wa Australia kuchaguliwa mwezi Mei.

Soma zaidi:Marekani yaahidi ushirikiano Indo-Pasifiki 

Wawili hao walikutana kwa mara ya kwanza mjini Tokyo, siku mbili baada ya uchaguzi wa Australia, katika Mazungumzo ya Usalama ya muungano unayojulikana zaidi kama Quad, ambayo yaliwaleta pamoja Albanese na Kishida pamoja na Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi.

Uamuzi huo wa kufanya mkutano wa Jumamosi huko Perth ilikuwa ishara ya uhusiano wa karibu wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

Makubaliano ya usalama wa nishati

Australien | Anthony Albanese
Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese.Picha: Martin Ollman/Getty Images

 Australia na Japan zimekubaliana pia kushirikiana katika suala la usalama wa nishati, ambalo linatishiwa kimataifa kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Australia hutoa kiwango kikubwa cha nishati kwa Japan ikiwa ni pamoja na gesi ya LNG na makaa ya mawe. Nchi zote mbili zimekubaliana kuhusu kuachana na uzalishaji wa gesi chafu ifikapo mwaka 2050.

Kishida na Albanese wamesema kuwa na nia ya dhati ya upokonyaji silaha za nyuklia. Kishida amesema shambulio la nyuklia la Urusi dhidi ya Ukraine litakuwa "tendo la uadui dhidi ya ubinadamu", na kuongeza kuwa kitendo cha Urusi kutishia matumizi ya silaha za nyuklia ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa na hakikubaliki kabisa.

Soma zaidi: Marekani, Uingereza na Australia zazindua muungano wa usalama

Nchi hizo mbili pia zilitia saini ubia muhimu wa madini ambao utaimarisha ugavi kwa watengenezaji wa vifaa wa Japan.

Bajeti ya ulinzi ya China imeongezeka kwa zaidi ya mara nne tangu mwaka 2007 wakati Australia na Japan zilipotia saini makubaliano yao ya kwanza ya ulinzi.

Mnamo mwaka 2006, ndege za kivita za Japan ziliruka mara 22 ili kuzuia ndege za kijeshi za China katika anga ya Japan. Mwaka jana ndege za kivita za Japan ziliruka mara 722 kuzuia uchokozi wa ndege za China.