1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Japan, US, Ufilipino zajiimarisha Bahari ya Kusini mwa China

4 Novemba 2023

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida amesema nchi yake, Marekani na Ufilipino zinashirikiana ili kulinda uhuru wa Bahari ya Kusini mwa China. Kishida ameyasema hayo wakati wa ziara yake, mbele ya bunge mjini Manila.

https://p.dw.com/p/4YOj3
Meli ya kijeshi ya China ikilinda doria Bahari ya Kusini mwa China
Meli ya kijeshi ya China ikilinda doria Bahari ya Kusini mwa ChinaPicha: Ted Aljibe/AFP

Waziri Mkuu Kishida  amyeyazungumza hayo akionesha dhamira yake ya kusaidia kuimarisha uwezo wa kiusalama wa Ufilipino. Mapema Ijumaa, Waziri Mkuu huyo wa Japan  na rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos Junior walikubaliana kuanzisha mazungumzo kuhusu mkataba wa wanajeshi wa pamoja kwa ajili ya kuongeza ushirikiano wa kijeshi wakati China ikiendelea pia kujiimarisha kwenye ukanda huo.

Soma zaidi: Manila yasema meli za China ziligonga kwa makusudi boti za Ufilipino

Manila na Tokyo ambazo ni washirika wa karibu wa Marekani zimekuwa na msimamo mkali dhidi ya kile zinachokiona kuwa ni tabia ya uchokozi ya meli za China katikati ya mvutano wa miaka mingi juu ya uhuru wa mipaka ya bahari. Beijing imekuwa ikidai kuwa na mamlaka juu ya karibu eneo zima la bahari ya Kusini mwa China yakiwemo maeneo muhimu ya kiuchumi ya Brunei, Indonesia, Malaysia, Ufilipino na Vietnam. Hata hivyo, mnamo mwaka 2016, mahakama ya kudumu ya usuluhishi ilisema kuwa, madai ya China hayana msingi wa kisheria.