1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jaribio la mapinduzi lazimwa Uturuki zaidi ya 250 wauwawa

16 Julai 2016

Vikosi tiifu kwa rais wa Uturuki vimezima jaribio la mapinduzi usiku wa Ijumaa (15.07.2016) kufuatia mashambuliano ya risasi yaliyohusisha pia ndege za kivita na kugharimu maisha ya zaidi ya watu 250.

https://p.dw.com/p/1JQ4x
Picha: Reuters/M. Sezer

Kufuatia upinzani wa umwagaji damu kwa utawaka wake wa miaka 13 Rais Recep Tayyip Erdogan amewataka wafuasi wake kuendelea kubakia mitaani kuzuwiya kuibuka upya kwa machafuko ya Ijumaa usiku (15.06.2016) katika nchi hiyo mwanachama muhimu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO.

Baada ya kukamatwa kwa takriban wanajeshi 2,839 katika msako wa waliohusika na njama hiyo ya mapinduzi serikali inamtupia lawama Sheikh Fethullah Gulen anayeishi Marekani ambaye ni hasimu mkuu wa Erdogan kwa kuhusika na njama hiyo ya mapinduzi.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema Jumamosi kwamba Marekani itaisaidia Uturuki katika uchunguzi kuhusu jaribio hilo la mapinduzi lililoshindwa na imeitaka serikali ya nchi hiyo kuwasilisha ushahidi ilio nao dhidi ya sheikh huyo anayeishi Marekani.

Doa jeusi kwa demokrasia

Waziri Mkuu Binali Yildrim amesema akiwa nje ya ofisi zake mjini Ankara akiandamana na mkuu wa majeshi wa Uturuki ambaye mwenyewe alikuwa akishikiliwa mateka na wahusika wa njama hiyo kwamba "serikali inaidhibiti hali hiyo kikamilifu.

Waziri Mkuu wa Uturuki Binali Yildirim.
Waziri Mkuu wa Uturuki Binali Yildirim.Picha: Reuters/Prime Ministry Pool

"Akilielezea jaribio hilo la mapinduzi kuwa ni "doa jeusi" kwa demokrasia ya Uturuki Vildrim amesema watu 161 wameuwawa katika machafuko hayo ya usiku na wengine 1,400 wamejeruhiwa.

Idadi hiyo inaonekana kutojumuisha wanajeshi101 walioasi waliouwawa usiku na hiyo kufanya jumla ya watu waliouwawa katika mchafuko hayo kufikia 265.

Wakati madaraka ya nchi yalipokuwa mashakani wakati wa usiku umati mkubwa wa watu wafuasi wa chama tawala cha Haki na Maendeleo (AKP)cha Rais Erdogan waliokuwa wakipeperusha bendera walikaidi amri ya kutotoka nje na kuandamana mitaani kuzuwiya jaribio hilo la kuipinduwa serikali.

Erdogan alitumia mtandao wake wa Twitter kuwahimiza watu wajitokeze mitaani kuhakikisha hakuna upinzani zaidi kwa madaraka yake.

Hali ilivyokuwa

Wakati kulipokucha picha za televisheni zilionyesha uharibifu mkubwa wa jengo la bunge mjini Ankara ambalo lilishambuliwa na ndege za kivita za wanajeshi walioasi.

Umma uliojitokeza kupinga jaribio la mapindzzi nje ya uwanja wa ndege wa Istanbul.
Umma uliojitokeza kupinga jaribio la mapindzzi nje ya uwanja wa ndege wa Istanbul.Picha: Reuters/H. Aldemir

Jaribio hilo la mapinduzi la Ijumaa lilianza kwa ndege za kivita chapa F-16 kuruka chini chini katika mji mkuu wa Ankara na wanajeshi na vifaru kuingia mitaani mbapo milio ya miripuko ilihanikiza usiku kucha katika mji mkuu huo pamoja na katika mji mkubwa kabisa nchini humo wa Istanbul.Ndege za kivita za jeshi la Uturuki chapa F-16 zilifanya mashambulizi ya anga dhidi vifaru vilivyowekwa na wahusika wa njama ya mapinduzi nje ya kasri la rais mjini Ankara.

Wakati umma ulipowageukia wanajeshi kadhaa waliokuwa wakiunga mkono mapinduzi hayo walisalimu amri karika daraja la Bosphorus mjini Istanbul waliokuwa wakilishikilia wakati wa usiku ambapo picha za televiheni zimewaonyesha wakinyoosha mikono yao juu kuashiria kusalimu amri wakati wakitiwa nguvuni.

Wahusika kukiona cha moto

Erdogan amelaani jaribio hilo la mapinduzi kuwa ni usaliti kwa taifa na kwamba wahusika watalipa kwa gharama kubwa kwa kitendo chao hicho cha uhaini.

Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki.
Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki.Picha: Reuters/H. Aldemir

Sheik Gulen rafiki aliyegeuka kuwa hasimu wa Erdogan anayetuhumiwa kuhusika na njama hiyo amekanusha vikali kuhusika kwa njia yoyote ile na njama hiyo kwa kusema kwamba tuhuma hizo dhidi yake ni "matusi".

Uturuki imetaka kurudishwa nchini humo kwa watu wanane wanaodaiwa kuhusika na njama hiyo ya mapinduzi ambao wamewasili Ugiriki kwa kutumia helikopta ya kijeshi chapa ya Black Hawk.

Dunia yataka kuungwa mkono kwa serikali

Viongozi wa dunia wametowa wito wa kuwepo utulivu nchini humo ambapo Rais Barack Obama wa Marekani na nchi nyengine za magharibi wamehimiza kuungwa mkono kwa serikali ya nchi hiyo ambayo wamesema imechaguliwa kwa njia ya demokrasia.

Maelfu waandamana Ankara kulaani jaribio la mapinduzi.
Maelfu waandamana Ankara kulaani jaribio la mapinduzi.Picha: Getty Images/AFP/A. Altan

Kiongozi wa Jumuiya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amekaribisha kile alichokiita "uungaji mkono madhubuti ulioonyeshwa na wananchi na vyama vya kisiasa kwa demokrasia na kwa serikali ilioyochaguliwa kidemokrasia ya Uturuki mwanachama muhimu wa Jumuiya ya NAO."

Msemaji wa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema "inapaswa kuchukuliwa hatua zote kuhakikisha maisha ya binaadamu yanalindwa" wakati waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault amesema anataraji demokrasia ya Uturuki "itaibuka ikiwa madhubuti zaidi.

Jeshi la Uturuki ambalo liliwahi kuwa na ushawishi mkubwa nchini humo kwa muda mrefu limekuwa likijihesabu kama mlezi wa taifa hilo lilisilo jifungamanisha katika misimamo ya kidini lililoasisiwa na Kemal Ataturk hapo mwaka 1923.Jeshi liliwahi kufanya mapinduzi mara tatu nchini humo tokea mwaka 1960 na iliiondowa madarakani serikali ya sera kali za Kiislamu hapo mwaka 1997.

Mwandishi : Mohamed Karama/ AFP/AP

Mhariri : Slyvia Mwehozi