1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Javier Solana atembelea askari wa Umoja wa Ulaya walioko Darfur

Kalyango Siraj7 Mei 2008

Msimu wa mvua unaokaribia utawapa taabu

https://p.dw.com/p/DvqI
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Javier Solana. Ametembelea vikosi vya Umoja wa Ulaya vilivyoko Afrika kulinda wakimbizi wa DarfurPicha: AP

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya,Javier Solana yuko barani afrika katika ziara rasmi ya kutembelea mataifa kadhaa ambayo yanahusika na mgogoro wa Darfur.

Javier Solana aliwasili katika mji mkuu wa Chad, N'Djamena, jana akitokea Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambako pia kuna majeshi ya Umoja wa Ulaya.

Afisa huyo wa yuko Chad kujionea mwenyewe kazi ngumu inayokikabili kikosi cha Umoja wa Ulaya cha kulinda wakimbizi wa Darfur.

Mauaji ya wiki iliopita ya mkuu wa shirika la kuwahudumia watoto la Uingereza la Save the Childrens Fund,yaliyotokea umbali wa kilomita tisa kutoka katika makao ya kikosi cha Umoja wa Ulaya,ni ishara moja ya kuwa hali inayokikabili kikosi hicho ni ngumu kweli.

Amekwenda katika sehemu inayoitwa Camp Europa,ambako ndiko kuna makao makuu ya kikosi hicho.Baadae aliruka kwa ndege hadi Abeche eneo lililoko katika mpaka wa Chad na Sudan.

Huko sio tu amekagua askari wa kikosi hicho lakini pia amejionea mwenyewe hali ya wakimbizi ilivyo.

Mwishoni mwa juma mashirika ya kutoa misaada yalisimamisha kwa mda wa siku mbili shughuli za utoaji msaada yakipinga kuuawa kwa afisa wa shirika la misaada ambako ni kwa mara ya tano mwaka huu.

Pia amekutana na wajumbe wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya kibinadamu OCHA pamoja na wajumbe wa mashirika mengine yasio ya kiserikali.

Kikosi cha Umoja wa Ulaya kilipewa idhini ya kwenda huko chini ya azimio la Umoja wa Mataifa mwaka jana,kwa lengo la kuwasaidia wakimbizi wa Darfur wa kutoka Sudan ambao wako Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Vile vile kikosi hicho kinajukumu la kuwalinda na kuwasaidia raia wa Chad pamoja na wa Jamhuri ya Afrika ya Kati,ambao wanasumbuliwa na mapigano ya ndani mwa nchi hizo wanaofikia laki nne Unusu.

Umoja wa Mataifa umesema mwezi uliopita kuwa, idadi ya watu waliofariki katika Darfur kutokana na mapigano,njaa na magonjwa, kwa kipidi cha miaka mitano, wanafikia laki tatu.

Hata hivyo utawala wa Khartoum unasema kuwa idadi yao ni ndogo kuliko hiyo inayosemwa na Umoja wa Mataifa.

Kikosi cha Umoja wa Ulaya kulichelewa kuanza kazi zake huko Chad kutokana na sababu kadhaa mkiwemo mjadala mrefu ndani mwa Umoja huo kuhusu askari watoke wapi, pamoja na hujuma za waasi walioushambulia mji wa N'Djamena wakiwa na nia ya kumuondoa madarakani rais Derby.

Kikosi hicho kilianza kazi zake rasmi Machi 17,na msemaji wa Solana anasema kuwa, kikosi hicho kinatarajiwa kuchapuza shughuli zake katika kipindi cha wiki chache zijazo kabla ya msimu wa mvua kuanza mwezi Juni.

Kati ya askari wote elf tatu na mia saba wanaohitajika, kwa sasa kuna wanajeshi elf mbili ,mia tatu na sabini na tisa ambao wametoka Ufaransa,Sweden na Ireland.