1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je Mugabe atajiuzulu?

John Juma
20 Novemba 2017

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amepewa muda wa hadi saa sita adhuhuri majira ya Afrika Kusini kujiuzulu la sivyo chama tawala cha ZANU-PF kitaanza mchakato wa kumuondoa madarakani.

https://p.dw.com/p/2nvB1
Simbabwe Mugabe bei TV-Ansprache
Picha: picture-alliance/AP Photo

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amepewa muda wa hadi saa sita adhuhuri majira ya Afrika Kusini kujiuzulu la sivyo chama tawala cha ZANU-PF kitaanza mchakato wa kumuondoa madarakani. Hii ni baada ya kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 93  kushindwa kutangaza  kujiuzulu kwake  kinyume na ilivyotarajiwa wakati wa  hotuba yake ya kwanza kwa umma jana usiku tangu jeshi lilipotangaza kldhibiti mamlaka wiki iliyopita.

Rais Robert Mugabe anakabiliwa na kitisho cha kuondolewa  madarakani  na chama chake, baada ya kuwashangaza watu kwa kusisitiza kuwa ataendelea kushikilia madaraka licha ya jeshi kutwaa udhibiti wa mamlaka na pia licha ya kupewa hadi muda wa saa sita adhuhuri ya leo  kujiuzulu ili kumaliza utawala wake ambao umedumu kwa miaka 37.

Mapema leo, kulikuwa na umati wa waandamanaji katika chuo kikuu cha Zimbabwe mjini Harare wakimtaka Mugabe ajiuzulu.

Maveterani kuwasilisha kesi dhidi ya Mugabe

Chama cha maveterani wa vita vya ukombozi kikiongozwa na Chris Mutsvangwa(aliyeketi katikati)
Chama cha maveterani wa vita vya ukombozi kikiongozwa na Chris Mutsvangwa(aliyeketi katikati)Picha: Getty Images/AFP/J. Nijkizana

Chama cha maveterani wa vita vya ukombozi wa nchi hiyo ambacho kimekuwa na sauti kubwa kumtaka Mugabe ang'atuke, kimesema jeshi linapaswa kujiondoa ili kuwaruhusu wananchi pamoja na mchakatio wa siasa kumuondoa Mugabe mamlakani. Chris Mutsvangwa ambaye ni kiongozi wa maveterani amesema wataongoza maandamano zaidi dhidi ya Mugabe na pia wataelekea mahakamani kuwasilisha kesi  dhidi ya  Mugabe kushindwa katika majukumu yake. Mutsvangwa ameendelea kusema:

"Rais Mugabe aliwashangaza Wazimbabwe katika hotuba yake iliyopeperushwa katika televisheni usiku wa kuamkia leo, pale alipokwepa kutaja lolote kuhusu kujiuzulu, badala yake aliahidi kuongoza mkutano wa wajumbe wa chama tawala ZANU-PF mwezi ujao, hii ni licha kuwa chama hicho kilimuondoa  kama kiongozi hapo jana."

Je Mugabe alikwepa sehemu ya hotuba kuhusu kujiuzulu?

Rais Mugabe alipotoa hotuba yake Jumapili usiku
Rais Mugabe alipotoa hotuba yake Jumapili usikuPicha: Getty Images/AFP/Str

Kulikuwa na uvumi kuwa huenda Mugabe alisoma hotuba tofauti na ile aliyopaswa kuisoma au alikwepa baadhi ya sehemu za hotuba hiyo kuhusu kujiuzulu kwake. Mkaazi wa Harare Pastor Tawanda amesema Mugabe hana jingine ila kujiuzulu: "Bado tuna  matumaini, amenaswa vilivyo. hana pa kukimbilia. hana pakwenda ma ntunmajua wiki hii atajiuzulu. yale yalikuwa maneno  Mzee tu.kishona tunasema mtu mzima hawezi kutamka wazi hadharani na kukubali kuwa ameshindwa."

Katika tukio jengine mapema leo, shirika la habari la kimataifa la Marekani-CNN, limeripoti kuwa  Robert Mugabe amekubali kujiuzulu na kwamba hotuba ya kujiuzulu kwake tayari imeshaandikwa. Shirika hilo limeinukuu duru inayofahamu mazungumzo kati ya Mugabe na makamanda wa jeshi waliotwaa mamlaka wiki jana.

Katika makubaliano ya kujiuzulu, Mugabe na mkewe Grace watapewa kinga kamili dhidi ya kukamatwa.

Jana Jumapili, kamati kuu ya ZANU-PF ilimtangaza Emmerson Mnangagwa kama kiongozi wao mpya. Hatua ya Mugabe kumfuta kazi makamu wa  rais Emmerson  Mnangagwa  ili kufungua njia kwa mkewe kumrithi ndiyo ililisababisha jeshi kuingilia kati na kuchukua udhibiti wa mamlaka.

Mwandishi: John Juma/RTRE/AFPE/

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman