1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je Obama afanikiwa barani Ulaya?

Saumu Ramadhani Yusuf7 Aprili 2009

Wataalamu waichambua ziara ya Obama barani Ulaya

https://p.dw.com/p/HSCE
Rais Obama akitoa hotuba yake iliyoshangiliwa PraguePicha: AP

Wataalamu wa mambo wanasema kuwa ziara ya kwanza ya rais wa Marekani Barack Obama barani Ulaya imefanikiwa kwa kiasi kidogo tu,lakini imempa nafasi ya kuwasilisha na kuonyesha haiba yake katika jitihada za kutafuta kuupunguza mgawanyiko unaondelea katika uhusiano wa Marekani na Ulaya.

Mkutano wa wiki iliyopita wa nchi za kundi la G20 mjini London ulifungua njia ya mpango wa dolla Trillioni moja kwa ajili ya kuufufua uchumi lakini Ujerumani na Ufaransa pamoja na nchi nyingine kadhaa za Umoja wa Ulaya zenye nguvu za kiuchumi zilijitenga na miito iliyotolewa na Marekani na Uingereza juu ya kutaka fedha zaidi za kuufufua uchumi.

'Katika mkutano wa NATO mjini Strasburg ikulu ya Marekani iliweza kudai kwamba zimetolewa ahadi za kutolewa wanajeshi 5000 zaidi kwa ajili ya kwenda Afghanistan ingawa wanajeshi hao wengi wao hawatobakia kwa muda mrefu .

Obama in Straßburg
Baada ya mkutano wa kilele wa NATO Strasbourg, Ufaransa.Picha: AP

Kando na hayo hotuba ya rais wa Mareakni mjini Prague bila pingamizi iliwagusa wafuasi wake katika nchi hiyo lakini serikali za eneo hilo la Mashariki zimebakia kuwa na wasiwasi kwamba harakati zake za kutaka kuinyoshea mkono Urusi huku akizungumzia juu ya ulinzi wa makombora ni jambo litakalowaacha katika hali mbaya.Akiwa ziarani nchini Uturuki mjini Istanbul hotuba yake ilikubalika na wengi katika ulimwengu wa nchi za kiarabu lakini mwito wake wa kutaka Uturuki ikubaliwe kujiunga na Umoja wa Ulaya ni suala lililowakasirisha sana wafaransa na mwito huo hautatoa mchango mkubwa katika kulisogeza mbele lengo la Uturuki.

Bila shaka moja ambalo kila mtu ameliunga mkono ni wazo lake la kutaka ulimwengu uondokane na sialaha za kinuklia lakini hata yeye mwenyewe binafasi amekiri kuwa ni jambo ambalo halitawezekana katika kipindi cha muda mfupi hasa ikizingatiwa nchi kama Korea Kaskazini ndo kwanza zinafanya majaribio ya makombora yake wakati Iran ikiendelea kurutubisha madini yake ya Uranium.Kwa wataalamu wengi barani Ulaya ambao wamezichambua hotuba za rais Obama juu ya sera zake za nje wanasema kwamba hazijaweka wazi tofauti na zile za mtangulizi wake George W Bush zilizokuwa zimewachukiza watu wengi.

Didier Billion Naibu mkurugenzi wa taasisi ya masuala ya kimataifa na uhusiano wa kimkakati anasema Obama ni mcheshi na mwenye mvuto mkubwa kuliko mtangulizi wake George Bush lakini anachokitetea ni maslahi ya Marekani na sio kinyume chake kwa hivyo ameonya kwamba wengi wa wafuasi wa Obama katika Ulaya wanajidanganya na watavunjwa moyo ikiwa walitarajia mabadiliko makubwa.

Katika mji wa Strassburg Ufaransa,Obama alifika bila ya kuwa na matarajio makubwa ya kuwashawishi washirika wa Marekani katika kuongeza wanajeshi katika mpango wake mpya nchini Afghanistan na badala yake alijaribu kutoa ombi moja kwa moja kwa umma kutokana na mikutano yake ya hadhara.

Hotuba yake ilitoa mabadiliko kidogo na matokeo ya mkutano huo wa kilele lakini ilishangiliwa na kupinga suara iliyojitokeza katika vyombo vya habari vilivyoonyesha maandamano ya upinzani ya watu wa mrengo wa kushoto wakichoma moto majengo na kuwavurumishia mawe polisi nje ya eneo la mkutano huo wa kilele.

Mbinu zake za kistadi katika siasa zimemfanya rais Obama kujikuta akituliza kitisho cha mgawanyiko na Uturuki ambayo ilipinga chaguo la Umoja wa Ulaya la atakayeongoza jumuiya ya Nato.Lakini yote tisa Kumi katika mapambano Afghanistan bado inabakia kuwa kuwa vita ambavyo Marekani inabidi kushinda au kushindwa.



Mhariri Mohammed Abdul-Rahman

Mwandishi Saumu Mwasimba/AFPE