1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je wenyeji Ufaransa watafurukuta mbele ya Wakorea?

Sylvia Mwehozi
7 Juni 2019

Pazia la Kombe la dunia la Wanawake linafunguliwa usiku wa Ijumaa mjini Paris, ambapo wenyeji Ufaransa wako katika shinikizo la kudhihirisha hadhi yao pale watakapovaana na Korea Kusini katika mechi ya ufunguzi.

https://p.dw.com/p/3K2ck
Top-Stars der Frauenfußball-EM | Amandine Henry aus Frankreich
Picha: picture-alliance/dpa/PH Renault

Ni mashindano makubwa ya kombe la dunia kwa wanawake kuwahi kufanyika ambapo karibu tiketi milioni moja tayari zimeuzwa kwa ajili ya michuano hiyo ambayo inatarajiwa kuleta msisimko mkubwa kwasababu kila timu iliyofuzu inawania kuchukua kikombe.

Kwa mujibu wa rais wa shirikiso la soka duniani Gianni Infantino, tiketi za mechi ya ufunguzi baina ya wenyeji na Korea Kusini zmemalizika na hivyo kuleta msisimko zaidi kwa wapenzi wa soka.Diane Gobert ni mmoja wa mashabiki anayesubiri kipenga kulia.

"Ndio ninafuatilia sana kombe la dunia kwasababu mimi ni mwanamke na kwasababu pia mpira ni kitu kikubwa Ufaransa. Nitatilia mkazo na pia nimenunua tiketi kwa ajili ya mechi mojawapo hapo Juni 16 kati ya Mexico na Marekani, kwasababu sitaweza kuwaona Ufaransa wakicheza moja kwa moja, lakini nitafuatilia timu ya Ufaransa kupitia vyombo vya habari na kwenye televisheni".

Fifa Fußball Damen Weltmeisterschaft 2015 Deutschland gegen England Edmonton Kanada
Baadhi ya wachezaji wa kikosi cha UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/Carmen Jaspersen

Timu ya Ufaransa itapata fursa ya kuonyesha uwezo wao wakati watakapotapotimua vumbi mbele ya umati wa mashabiki 47,000 katika dimba la Parc des Princes dhidi ya Wakorea. Timu hiyo ya Ufaransa chini ya nahodha wake Amandine Henry iko kundi A ambalo pia linajumuisha timu za Norway na Nigeria. Kikosi hicho cha Les Bleues ambacho kiko nafasi ya nne katika viwango vya ubora vya FIFA kinapewa nafasi ya pili baada ya Marekani ambao ni mabingwa watetezi. Soma zaidi...

Timu ya wanawake ya Ufaransa inataka kupata mafanikio sawa na wenzao wa kiume ambao ndio mabingwa wa sasa wa dunia. Korea Kusini ililala bao 3-0 dhidi ya Ufaransa katika hatua ya 16 bora wakati wa kombe la dunia la 2015 lililofanyika nchini Canada na safari hii ingetamani kufikia hatua za mtoano kwa mara nyingine tena. Marekani inatafuta kunyakua taji hilo kwa mara ya nne huku Ujerumani itakayokipiga na China katika mechi za kundi B siku ya Jumamosi nayo ikikitolea macho kikombe hicho. Hispania inawakaribisha Banyanabanyana ya Afrika Kusini katika kundi B. Michuano hiyo ya kombe la dunia kwa wanawake itachezwa katika majiji tisa ndani ya Ufaransa huku tiketi za nusu fainali na fainali zikiwa tayari zimemalizika.

AFP