1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JEDDAH:Viongozi wa Somalia watia saini makubaliano ya maridhiano

17 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBP7

Viongozi wa serikali ya muda ya Somalia inayoungwa mkono na majeshi ya Ethiopia wametia saini makubaliano ya maridhiano baada ya mkutano wa maridhiano ya kitaifa kutofikia mwafaka wowote.Mkutano huo ulifanyika mwezi jana mjini Mogadishu.

Bado haijulikani kilichoafikiwa katika makubaliano hayo.Mkutano wa maridhiano wa mwezi jana ulimalizika bila maafikiano yoyote jambo lililowafanya wanadiplomasia wa kigeni kutoa wito wa kuchukua hatua za kuwaleta pamoja wahusika ili kumaliza ghasia zinazozonga nchi ya Somalia tangu kungolewa madarakani kwa Rais Mohamed Siad Barre mwaka 91.

Rais Abdullahi Yusuf Ahmed,Waziri Mkuu Ali Mohamed Gedi na spika wa Bunge Sheikh Aden Mohamed Nur walihudhuria mkutano huo wa Jedda nchini Saudia.

Saudia inatoa wito kwa wahusika wote kuheshimu makubaliano hayo na kuunga mkono kauli ya Rais wa Somalia iliyoeleza kuwa majukumu ya majeshi ya kigeni yatatimizwa na majehsi ya kiArabu na Afrika chini ya mwamvuli wa Umoja wa mataifa kuhakikisha usalama unadumishwa.

Somalia kwa upande wake inaridhia kupelekwa kwa majeshi ya Kiarabu na Kiafrika yatakayosimamiwa na Umoja wa mataifa.Kikao cha mwezi jana kilisusiwa na wawakilishi wa mahakama za kiislamu waliofanya mkutano wao nchini Eritrea wiki jana.Eritrea ni adui wa nchi ya Ethiopia inayounga mkono serikali ya muda Somalia.Somalia ni mwanachama wa Jumuiya ya Milki za Kiarabu iliyo na nchi 22 wanachama.