1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Israel latibua shambulizi la Hamas baharini

Josephat Charo
25 Oktoba 2023

Jeshi la Israel limesema wapiganaji wa kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza walijaribu kujipenyeza na kuingia Israel kupitia baharini. Milio imesikika na wanamgambo kadhaa wameuwawa.

https://p.dw.com/p/4Xzct
Israel Aschkelon Truppenaufmarsch am Gazastreifen
Israel imeendelea kupeleka wanajeshi katika kijiji cha Zikim kibbutz huko Ashkelon katika eneo la mpaka na Gaza.Picha: Mostafa Alkharouf/Anadolu/picture alliance

Jeshi la Israel limesema wapiganaji wa kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza walijaribu kujipenyeza na kuingia Israel kupitia baharini. Vikosi vya wanamaji viligundua wapiga mbizi waliotumwa na kundi hilo linalotambuliwa kuwa la kigaidi nchini Ujerumani, Marekani na Umoja wa Ulaya, na kulizima shambulizi lao. Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la Israel wapigambizi wa Hamas walikuwa wamepanga kuvuka upande wa kaskazini kupitia pwani hadi katika kijiji cha mpakani cha Zikim kibbutz, na kwa sasa vikosi vya jeshi vinafanya msako katika eneo hilo.

Vyombo vya habari vya Israel vimesema milio ya risasi imesikika na wanamgambo kadhaa wameuwawa. Jeshi la Israel limesema limeushambulia uwanja wa kijeshi katika Ukanda wa Gaza ambao wanamgambo walikuwa wameutayarisha.

Wakati haya yakiarifiwa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito mapigano yasitishwe mara moja Gaza. Guterres ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa mashambulizi dhidi ya Gaza yanakiuka sheria ya kimataifa. Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa Gilad Erdan amejibu kauli hiyo kwa kumtaka Guterres ajiuzulu, akimtuhumu kwa kuonyesha kuelewa na kukubaliana na ugaidi na mauaji katika mashambulizi ya Hamas mnamo Oktoba 7.

Katika matamshi aliyoyatoa kwa Baraza la Usalama jana Jumanne, Guterres alikosoa ukiukaji wa wazi wa sheria ya kimataifa unaoshuhudiwa Gaza. Alisema Wapalestina wamekabiliwa na ukaliaji wa miongo kadhaa, kabla kuongeza kwamba ni muhimu kutambua mashambulizi yaliyofanywa na Hamas hayakufanyika katika ombwe.

Erdan aliandika katika ukurasa wake kwenye mtandao wa X, zamani Twitter na akasema kauli za Guterres zina maana hafai kuuongoza Umoja wa Mataifa.

USA New York | UN-Sicherheitsrat | Debatte über Nahost | Antonio Guterres, Generelsekretär
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Seth Wenig/AP Photo/picture alliance

Matamshi ya Guterres pia yamemghadhabisha waziri wa mambo ya nje wa Israel Eli Cohen ambaye amemnyoshea kidole cha lawama Guterres na kupaza sauti yake akielezea jinsi raia, wakiwamo watoto wadogo, walivyouliwa Oktoba 7. Cohen alifuta mkutano uliokuwa umepangwa kati yake na Guterres baada ya malumbano hayo. Cohen aliandika akisema hatakutana na katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa. "Baada ya Oktoba 7 hakuna mtazamo wenye uwiano. Hamas lazima iangamizwe kabisa katika uso wa dunia".

Macron akutana na Abbas Ukingo wa Magharibi

Wakati haya yakiarifiwa, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameutembelea Ukingo wa Magharibi ambako alikutana na Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas, jana Jumanne. Wakati wa mazungumzo hayo, Macron alisema kundi la Hamas haliwawakilishi Wapalestina. Abbas ameiongoza mamlaka ya ndani ya Wapalestina kwa miaka 18, huku ikidhibiti maeneo fulani ya Ukingo wa Magharibi na Hamas wakitawala Ukanda wa Gaza.

Rais Abbas amemhimiza Macron akomeshe ushambuliaji akizungumzia harakati za kijeshi za Israel kuelekea Gaza. Abbas ametoa wito kufanyike mkutano wa amani wa kimataifa kuhusu Gaza huku akikosoa mashambulizi ya kutokea angani ya Israel yanayoua raia wasio na hatia. Macron kwa upande wake alisema mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7 nchni Israel pia ni janga kwa Wapalestina. Macron pia alisema hakutakuwa na amani yoyote ya kudumu ikiwa hakutakuwa na utambuzi wa wazi kutoka kwa Wapalestina na mamlaka zao kwa taifa la Israel na umuhimu wa taifa hilo kuwepo pamoja na usalama wake.. 

Soma pia: Mateka wawili waachiwa na kundi la Hamas

Kwingineko Umoja wa Mataifa umesema hakuna msaada wowote ulioingia Gaza jana Jumanne. Umoja huo unasema malori 20 yaliyokuwa yapeleke msaada kupitia kivuko cha Rafah kutokea Misri hayakuingia Gaza kama ilivyopangwa. Msemaji wa Umoja wa Mataifa Eri Kaneko amesema wanatumai msaada utaweza kuingia Gaza leo Jumatano.

Tangu Jumamosi iliyopita malori 54 yamevuka na kuingia Gaza yakibeba vyakula, dawa na maji, huku katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiueleza msaada huo kama "tone kwenye bahari ya mahitaji".