1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Nigeria laua wapiganaji wa Boko Haram

Caro Robi18 Mei 2013

Ndege za kivita za Nigeria zimeshambulia kambi za wanamgambo wa Boko Haram kaskazini mashariki mwa nchi hiyo katika mapambano makubwa na kuzua onyo kali kutoka Marekani la kuheshimu haki za binadamu.

https://p.dw.com/p/18aEt
Wanajeshi wa Nigeria
Wanajeshi wa NigeriaPicha: Reuters

Wanajeshi wametumia ndege na helikopta kushambulia ngome za Boko Haram katika operesheni kubwa ya kijeshi tangu kundi hilo lilipoanzisha mapambano miaka minne iliyopita likitaka kuanzisha serikali ya misingi ya Kiislamu.Duru za jeshi zinaarifu kuwa karibu wapiganaji 30 wameuawa.

Siku tatu baada ya Rais Goodluck Jonathan kutangaza hali ya hatari nchini Nigeria katika maeneo ya kaskazini mashariki,waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ametoa taarifa ya onyo kali inayosema kuwa nchi yake ina wasiwasi kuhusiana na madai kuwa maafisa wa usalama wanakiuka haki za binadamu ambapo hali hiyo inaweza ikachochea zaidi ghasia na itikadi kali.

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan atangaza hali ya hatari
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan atangaza hali ya hatariPicha: Pius Utomi Ekpei/AFP/Getty Images

Marekani ndiyo mwekezaji mkubwa wa kigeni nchini Nigeria hasa katika sekta ya kawi na inanunua thuluthi moja ya mafuta ya taifa hilo la magharibi mwa Afrika.Kerry amesema Marekani inalaani vikali vitendo vya kigaidi vya Boko Haram lakini amelihimiza jeshi nchini humo kuonyesha hali ya kujizuia na kudumisha nidhamu wakati wa operesheni dhidi ya kundi hilo.

Kambi na silaha za waasi zaharibiwa

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Nigeria Brigadier Jenerali Chris Olukolade amesema wanajeshi wameharibu kambi kadhaa za Boko Haram na shehena ya silaha katika misitu katika jimbo la Borno ambalo ni kitovu cha ghasia.

Olukolade amesema silaha nzito zikiwemo za kudungua ndege na bunduki za kushambulia vifaru vya kijeshi zimeharibiwa katika operesheni hiyo na kuongeza kuwa idadi kamili ya waasi waliouwawa itatolewa wakati wa zoezi la kusaka kambi hizo ikiwemo mbuga ya wanyama pori la Sambisa katika jimbo la Borno.

Majeshi ya Nigeria yanajaribu kudhibiti ngome za Boko Haram katika majimbo ya Borno,Yobe na Adamawa ambayo yamewekwa chini ya hali ya hatari na Rais Jonathan siku ya Jumanne wiki hii.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John KerryPicha: Reuters

Wapiganaji hao wa Kiislamu wenye itikadi kali wamekuwa tishio kubwa kwa usalama wa taifa hilo linalozalisha mafuta , kwa kuongeza mashambulizi yao tangu mwezi uliopita likiwemo shambulio katika mji wa Bama lililosababisha vifo vya watu 55.

Hofu ya kugawanyika kwa Nigeria

Maafisa nchini Nigeria wanahofia kuwa waasi hao wa Boko Haram wanataka kuunda nchi ndani ya nchi kama jinsi wanamgambo walio na mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda walivyotaka kufanya nchini Mali kabla ya majeshi ya Ufaransa kukabilana nao mwezi Januari.

Hata hivyo juhudi za hapo awali za kukomesha shughuli za Boko Haram zimekuwa za kutuliza hali kwa muda tu zinazowafanya waasi hao kujificha na kuvuka mipaka ambako wanasubiri, na kisha wanajikusanya tena na kurejea Nigeria.

Wanajeshi zaidi waliwasili Ijumaa katika mji mkuu wa jimbo la Borno,Maiduguri ambako ni chimbuko la kundi hilo ambalo lilianza kama vuguvugu la kidini linalopinga mila na desturi za mataifa ya magharibi lakini baada ya shambulio la kijeshi dhidi yao ambapo watu 800 waliuwawa,lilijigeuka na kuwa kundi kamili la waasi na kufungamana na makundi yaliyo na mafungamano na Al Qaeda katika eneo la jangwa la Sahara.

Mwandishi:Caro Robi/Reuters/ap

Mhariri:Sekione Kitojo.