1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Venezuela laendeleza utii kwa Maduro

Lilian Mtono
20 Februari 2019

Waziri wa ulinzi wa Venezuela Vladmir Padrino amesisitiza kwamba jeshi nchini humo linalomtii rais Nicolas Maduro, litaendelea kuimarisha hali ya tahadhari dhidi ya ukiukwaji wowote kwenye mipaka yake.

https://p.dw.com/p/3Djxd
Venezuela Caracas - Präsident Nicolas Maduro kommt zur Feierlichkeit des Army Day
Picha: picture-alliance/AP Photo/F. Llano

Hatua hii inakuja katika wakati ambapo mpinzani wa rais Maduro, Juan Guaido akiongeza shinikizo dhidi ya jeshi kuruhusu kuingia kwa misaada ya kibinadamu nchini humo. 

Amenukuliwa na gazeti la kila siku nchini humo la El Nacional akisema, jeshi lina rais mmoja tu, ambaye ni Maduro. Amesema halitaruhusu serikali ya kibaraka ama maagizo kutoka kwa serikali yoyote ya nje.

Ametoa matamshi hayo baada ya rais Donald Trump wa Marekani anayemuunga mkono Guaido kulionya jeshi la Venezuela siku ya Jumatatu kwamba watapoteza kila kitu iwapo wataendelea kumuunga mkono Maduro, na kuongeza kuwa watapendelea mabadilishano ya amani ya madaraka, lakini mapendekezo mengine yako mezani.

Venezuela, Urena: Tienditas International Bridge
Daraja linalounganisha Venezuela na Colombia, ni miongoni mwa maeneo yaliyofungwa na MaduroPicha: picture alliance/AP/F. Llano

Mapema, rais Maduro amehoji kwenye hotuba yake iliyorushwa na televisheni ya taifa, wakati akiwahutubia wahitimu wa chuo cha tiba akisema Guaido anayejiita rais wa mpito, Mbona haitishi uchaguzi ili wafuasi wake wamchague kwa kura!

Alisema "Sawa, kama ni rais wa mpito, kitu cha kwanza anachotakiwa kukifanya ni kuitisha uchaguzi. Mbona hajaitisha? Jiulizeni, kwa nini hajaitisha uchaguzi? Anayejiita rais wa mpito, mbona hajaitisha uchaguzi ili wafuasi wake wamchague kwa kura? Itisha uchaguzi rais uliyejitangaza kama una uthubutu."

Maduro arudia kusema Venezuela haina mzozo wa kibinaadamu.

Alirudia tena ujumbe wake kwa rais Trump kwamba Venezuela haina mzozo wa kibinaadamu, kufuatia mwito wa rais huyo wa kuruhusiwa kwa misaada kuingia nchini humo, ambayo hata hivyo ilizuiwa na jeshi la Venezuela.

Colombia imesema kwamba zaidi ya tani 200 za msaada wa dawa, chakula na vifaa vya usafi, nyingi miongoni mwake vikiwa vimetolewa na Marekani vimehifadhiwa katika mji wa mpakani wa Cucuta. Guaido aliapa kuingiza misaada kutoka maeneo mbalimbali kwa njia moja ama nyingine, licha ya vikwazo hivyo vya kijeshi. Misaada hiyo ilitarajiwa kuingia kupitia Brazil na kisiwa cha Curacao.

Hata hivyo, kulingana na gazeti la kila siku la El Universal, kamanda wa jeshi Vladimir Quintero aliwathibitishia waandishi wa habari baadae kwamba Venezuela imeagiza kufungwa mara moja kwa muda , njia za baharini na angani zinazoiunganisha Venezuela na Kisiwa cha Curacao na visiwa vingine jirani vya Antilles vilivyoko Uholanzi, vya Aruba na Bonaire.

Msemaji wa ikulu ya Venezuela amesema, taifa hilo linashirikiana na Marekani kuleta misaada nchini humo, lakini ingewaachia Wavenezuela wenyewe kuichukua kutoka mpakani.

Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE/AFPE

Mhariri: Sekione Kitojo