1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi laingilia kati Zimbabwe ambako hali inatatanisha

Oumilkheir Hamidou
15 Novemba 2017

Jeshi nchini Zimbabwe linawashikilia rais Robert Mugabe na mkewe na kuzilinda ofisi za serikali pamoja na kupiga doria katika mitaa ya mji mkuu Harare.Hali ya wasi wasi imetanda mji mkuu Harare

https://p.dw.com/p/2nelO
Simbabwe Krise Straßenszenen aus Harare
Picha: Reuters/P. Bulawayo

Vifaru vya jeshi la Zimbabwe vimezifunga njia kuelekea bungeni,  makao makuu ya chama tawala cha Zanu-PF na katika ofisi ambako kawaida rais Robert Gabriel Mugabe hukutana na mawaziri wake. Masaa machache kabla ya hapo, afisa mmoja wa ngazi ya juu wa kijeshi, Major jenerali Sibusiso Moyo alitangaza kupitia televisheni ya nchi hiyo kwamba jeshi limeingilia kati dhidi ya "wahalifu wanaomzunguka rais Mugabe, na kukanusha njama yoyote ya mapinduzi."Tungependa kulihakikishia taifa kwamba mheshimiwa, rais wa jamhuri ya Zimbabwe, mkuu wa vikosi vya wanajeshi wa Zimbabwe, komredi Robert Gabriel Mugabe na familia yake wako salama usalimina."

Rais R.G. Mugabe na mkewe Grace
Rais R.G. Mugabe na mkewe GracePicha: Reuters/P. Bulawayo

Wapi Mugabe amewekwa haijulikani

Major jenerali Sibusiso Moyo amesema lengo la kuingilia kati ni kuwaandama "wahalifu wanaomzunguka Mugabe". Haijulikani lakini wapi Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 93 na mkewe wamewekwa. Inaonyesha kana kwamba wanashikiliwa jeshini.

Wanajeshi wote wametakiwa warejee kambini haraka na walioomba kikizo wamekataliwa. Miripuko mitatu imesikika jana usiku mjini Harare.

Opereshini hizo za jeshi zinadhihirika zimelenga kudhdibiti hali ya mambo nchini humo. Mkuu wa vikosi vya wanajeshi Constantino Chiwenga alitishia jumatatu iliyopita "wataingilia kati" kusitisha mivutano ya kisiasa nchini. Chama tawala cha Zanu-PF kilijibu kwa kumtuhumu jenerali huyo kufanya uhaini.

Jeshi lakini linasifiwa na wazee waliopigania ukombozi kwa "kukomesha bila ya kumwaga damu, mitindo ya kutumiwa vibaya madaraka."Wanajeshi watairejesha Zimbabwe katika mfumo halisi wa kidemokrasi" na kuigeuza nchi iwe ya kimambo leo.

Watu wanapiga foleni benki kuchukua akiba zao
Watu wanapiga foleni benki kuchukua akiba zaoPicha: Reuters/P. Bulawayo

SADC iko tayari kupatanisha

 Ubalozi wa Marekani umefungwa na raia wa Marekani wametakiwa kubakia majumbani mwao. Onyo kama hilo limetolewa pia na Uingereza.

Nae rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ameelezea matumaini yake kwamba hakuna mageuzi ya kinyume na katiba yatakayotokea baada ya jeshi kudhibiti madaraka mjini Harare. Rais Zuma amewatolea wito serikali na jeshi wamalize tofauti zao kwa amani akiahidi jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika iko tayari kusaidia.

Hali ya wasi wasi imeenea huku wazimbabwe wakipiga foleni mbele ya benki zao kuchukua akiba wanazoruhusiwa kuchukua. Wengine, simu mkononi kujua yanayoendelea huku wakielekea madukani au kazini.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman