1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joto la kisiasa nchini Uganda

Saumu Ramadhani Yusuf7 Oktoba 2010

Upinzani nchini Uganda wasema unapanga kuzuia wizi wa kura katika uchaguzi mkuu ujao

https://p.dw.com/p/PYio
Kiongozi wa Upinzani Kizza BesigyePicha: dpa

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Uganda Kizza Besigye amesema chama chake kinapanga kuchukua hatua ya kipekee ya kulinganisha matokeo ya uchaguzi baada ya kura kuhesabiwa katika uchaguzi mkuu wa mwakani.Hatua hiyo ya Upinzani inaonekana kama ni changamoto ya moja kwa moja dhidi ya serikali pamoja na shinikizo za rais Museveni za kukataa kufanya mageuzi katika tume ya Uchaguzi nchini humo. Chama cha muungano wa upinzani nchini Uganda kinapanga kuweka mawakala wake maalum katika kila kituo cha kupigia kura kote nchini Uganda katika uchaguzi mkuu wa rais na bunge mnamo mwakani katika juhudi za kukabiliana na kile inachokitaja wizi wa kura unaofanywa na serikali katika chaguzi zilizopita.

Wahlen in Uganda Yoweri Museveni
Wafuasi wa rais Yoweri Museveni katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2006Picha: AP

Mawakala hao kwa mujibu wa kiongozi wa muungano huo wa upinzani Kiza Besigye watawajibika katika kutuma kwa njia ya simu matokeo ya kura kutoka kvituo mbali mbali nchini humo hadi kwenye kituo kikuu cha kutangaza matokeo rasmi. Upinzani unasema hatua hiyo ni ya aina yake kuwahi kufanyika nchini Uganda, kama alivyofafanua msemaji wa muungano huo wa Interparty Cooperation Coalition Semjuu Ibrahim akisema-

''Kitu kipya hapa ni kwamba awali hatukuwa na miundo mbinu ya kutuwezesha kuchukua hatua hii lakini sasa tumejipanga na tutakuwa tunapata hesabu kamili ya matokeo ya kura kwa njia ya simu na kuyatangaza''

Serikali ya Uganda imesema kwamba Tume ya Uchaguzi ndio chombo pekee kinachoruhusiwa kikatiba kutangaza matokeo ya uchaguzi na hatua hiyo ya Upinzani haiwezi kukubaliwa.

Lakini upande mwingine upinzani ukitolea mfano wa kile kilichotokea nchini Kenya baada ya Tume ya Uchaguzi ya ECK kutangaza matokeo kufuatia madai ya kushinikizwa na serikali,Umesema utajitahidi kile uwezavyo kuwatangazia wananchi wa Uganda matokeo licha ya kupewa onyo na rais Museveni-

''Tume ya uchaguzi inamtangaza mshindi na aliyeshindwa na kama ilivyotokea huko Kenya sisi pia bila shaka wafuasi wetu wanahaki ya kupata maelezo kamili kwahivyo tutakapopata matokea tutakuwa tunawaambia haya ndio matokeo yetu''

Upinzani umemtolea mwito rais Museveni kuufuta kazi uongozi wa juu wa tume ya uchaguzi na kuteua tume ya muda lakini rais Museveni amelipinga pendekezo hilo akisema anaimani na uwezo wa tume ya sasa ya Uchaguzi.

Mahakama kuu ya Uganda wakati ikitoa hukumu yake kuhusu malalamiko ya upinzani katika chaguzi za mwaka 2001 na mwaka 2006ambapo Besigye aliupinga ushindi wa rais Museveni kwa madai kwamba ulitokana na wizi mkubwa wa kura pamoja na vitisho dhidi ya upinzani,ilisema kwamba tume ya uchaguzi ilishindwa kuendesha zoezi la uchaguzi kwa mujibu wa sheria,na kwamba ilionyesha upendeleo kwa kiasi kikubwa.

Aidha Besigye ambaye ni kiongozi wa chama cha Forum for Demokratic Change FDC amesema chama chake kinapanga kutangaza matokeo ya uchaguzi huo utakaofanyika Februari mwakani,kabla ya tume kutangaza.Je kwa umbali gani upinnzani unaweza ukafanikiwa katika mpango wake huo,Semjuu Ibrahim msemaji wa muungano wa vyama vya upinzani nchini Uganda anasema-

''Tumefanikiwa kupata matokeo halali katika maeneo bunge kwasababu wamejaribu kuiba kura lakini wakashindwa kwakuwa ni rahisi kuiba kura na kubadilisha matokeo wakati wakusafirisha masanduku ya kura katika vituo vya kutangaza matokeo''

Hata hivyo Tamale Mirundi msemaji wa rais Museveni akizungumza na shirika la habari la Reuters amesema hatua hiyo ya upinzani haitokubalika hata kidogo na kwamba Besigye anakichaa na kwa maana hiyo anaweza pia kuandaa uchaguzi wake mwenyewe wa kitaifa.Rais Museveni ambaye anataka kuwania kwa mara nyingine baada ya kuitawala Uganda kwa miaka 25 amekuwa akisifiwa sana na nchi za magharibi lakini sifa hizo zimetoweka huku wakosoaji wakimshutumu kuwa kiongozi aliyegeuka kuwa dikteta,fisadi na anayetafuta njia za kumuweka mwanawe wa kiume madarakani.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/RTRE

Mhariri:M.Abdul-Rahman