1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

JUBA:SPLM yajiondoa katika muungano wa kitaifa

12 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7GX

Wanachama wa kusini wa Sudan Peoples Liberation Movement, SPLM wamejiondoa katika serikali ya muungano wa kitaifa ili kuwashinikiza washiriki wa eneo la kaskazini kuchagiza makubaliano ya amani yaliyokwama.Hata hivyo kulingana na Katibu Mkuu wa SPLM Pagan Amum chama hicho hakijajiondoa serikalini na mawasiliano nao bado yako wazi.

Bunge linaendelea na shughuli zake aidha Bwana Salva Kiir anaendelea na wadhifa wake kama makamu wa rais wa Kwanza kutoka eneo la kusini mwa Sudan.Yasir Arman ni Naibu Katibu Mkuu wa SPLM

''Tunasubiri kauli ya muungano wa kitaifa….tuko tayari kukaa nao na kutafuta suluhu ya tatizo hili.Wanaendelea kukiuka makubaliano ya amani jambo linalohatarisha maafikiano hayo.Tunataka amani na ztumechukua hatua hii ili kujulisha jamii ya kimataifa kinachoendelea Sudan ..hatutaki vita.

Kwa mujibu wa Bwana Amum Chama cha National Congress NCP kilicho na wawakilishi wengi zaidi katika muungano huo kimeshindwa kutimiza sehemu ya vipengee vya makubaliano yaliyotiwa saini mwaka 2005.

Makubaliano hayo ya amani yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu muda mrefu zaidi barani Afrika na kuwezesha serikali ya muungano kuundwa mjini Khartoum.Chama cha SPLM kina robo ya nafasi zote serikalini.Makubaliano hayo aidha yanashughulikia ugavi wa mali vilevile kufanya matayarisho ya uchguzi unaopangwa kufanyika mwaka 2009 pamoja na kura ya maoni kuhusu eneo la kusini linalotaka kujitenga.Mazungumzo ya amani kuhusu eneo la Darfur yanapangwa kufanyika mjini Tripoli,Libya mwezi huu.