1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jubilee ina mawakala katika kamisheni ya IEBC, Odinga

13 Oktoba 2017

Upinzani nchini Kenya unasisitiza hakutokuwa na uchaguzi tarehe 26 Oktoba kama ilivyotangazwa na kamisheni inayosimamia uchaguzi nchini humo IEBC.

https://p.dw.com/p/2loCG
Kenia Nairobi Opposition ehemailger Präsident Raila Odinga
Picha: Reuters/B. Ratner

Haya ni licha ya kamisheni hiyo kusema itaanza kuchapisha makaratasi ya kupigia kura wiki hii pamoja na kufanya matayarisho mengine ya uchaguzi. Kiongozi wa muungano wa upinzani NASA Raila Odinga ambaye alitangaza kujiondoa kwenye mchakato huo wa kura, amesema kufanya uchaguzi kutakuwa ni kukiuka sheria. Odinga aliyasema haya Ijumaa katika mahojiano na DW huko London, Uingereza, ambako yuko ziarani.

Odinga alisema uamuzi wa mahakama ya juu ya Kenya katika ile rufaa ya kura ya rais ya mwaka 2013, uliweka wazi kuwa iwapo mgombea mmoja, iwe ni rais mteule au yule aliyekata rufaa, atajiondoa kwenye marudio ya uchaguzi basi hakutokuwa na uchaguzi.

Kiongozi huyo wa upinzani wa Kenya aliikosoa mahakama kuu ya Kenya iliyotoa uamuzi wa kujumuishwa katika uchaguzi mgombea wa chama cha Third Way Alliance Ekuru Aukot, akisema mahakama hiyo haina uwezo wa kuubadilisha uamuzi wa mahakama ya juu, kwani ndiyo iliyotoa uamuzi kwamba uchaguzi huo wa marudio ujumuishe wagombea wawili wakuu ambao ni yeye Raila Odinga na Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee.

IEBC inastahili kufanya kura za mchujo kwanza

Lakini usemi huu wa Odinga umetofautiana na ule alioutoa awali pale aliposema kwamba wagombea wote wanane wanastahili kushiriki marudio hayo ya kura ya rais.

Porträt - Dr. Ekuru Aukot
Mgombea wa chama cha Third Way Alliance Ekuru AukotPicha: KHK/GCR21/G. Lukas

"Kulingana na hali ilivyo kwa sasa, hakutokuwa na uchaguzi tarehe 26 Oktoba kwa mujibu wa sheria. Wanachofanya ni kujaribu kufanya uchaguzi lakini hilo haliwezi kufanyika," alisema Odinga. "Wanastahili kufanya kura mpya za mchujo. Uamuzi wa mahakama kuu ni knyume kwa kuwa mahakama hiyo haiwezi kuutengua uamuzi wa mahakama ya juu," aliongeza kiongozi huyo.

Mara baada ya Odinga kutangaza kujiondoa katika marudio ya uchaguzi, kamisheni inayosimamia uchaguzi nchini Kenya ilisema haitambui kujiondoa kwake ingawa kiongozi huyo sasa anasema aliwasilisha barua rasmi na kamisheni hiyo ikakiri kuipokea barua hiyo.

Jubilee ina mawakala wanaoitumikia IEBC 

Ingawa hakuwataja majina, kiongozi huyo wa NASA alidai kuwa serikali ya jubilee imeweka mawakala katika taasisi za kusimamia uchaguzi huku akisema upinzani umebaini makamishna 4 wa IEBC ambao wanaitumikia serikali katika taasisi hiyo.

Kenia nach der Annulierung der Präsidentenwahl | Uhuru Kenyatta
Uhuru Kenyatta ameshutumiwa na Odinga kuwa diktetaPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

"Ni serikali inayohitilifiana na kuwepo kwa uchaguzi huru na haki kwasababu wanataka kuchakachua matokeo ya uchaguzi," alisema Odinga. "Kwa hiyo unapata IEBC kwa sasa haiwezi kufanya kazi yake kwa njia huru."

Aliwataka Wakenya kusimama na kupigania uhuru na haki zao akiwashutumu rais Uhuru Kenyatta na William Ruto kuwa madikteta na kwmaba wanairejesha Kenya katika enzi za ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Mwandishi: Jacob Safari/DW

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman