1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi kuokowa mazungumzo ya Mashariki ya Kati

7 Aprili 2014

Juhudi za Marekani kuyanusuru mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati yasisambaratike zimeshindwa kupiga hatua kubwa huku kukiwa na vitisho kutoka Israel dhidi ya hatua za upande mmoja zinazochukuliwa na Wapalestina.

https://p.dw.com/p/1BdR9
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry .
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry .Picha: BRENDAN SMIALOWSKI/AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani na wa Kipalestina wajumbe wa upatanishi wa Israel na Palestina watakutana leo hii wakati Marekani ikiwa mbioni kuyaokowa mazungumzo hayo ya amani.

Afisa wa Palestina amesema mazungumzo ya jana usiku kati ya wajumbe wakuu wa usuluhishi Tzipi Livni wa Israel na Saeb Erakat wa Palestina yalikuwa hayana mvutano mkubwa kulinganishwa na mikutano yao ya nyuma.

Afisa wa Marekani ameuelezea mkutano huo kuwa ulikuwa makini na wenye tija.

Mazungumzo hayo yanafanyika wakati Wapalestina wakiomba kujiunga na mashirika na mikataba ya kimataifa na kuiudhi Israel ambayo inaiona hatua hiyo kama ni jaribio la kutaka utambuzi wa taifa lao bila ya kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na taifa hilo la Kiyahudi.

Kukwama kwa mazungumzo

Mazungumzo hayo ya amani yalioanza hapo mwezi wa Julai mwaka jana yamekwama kutokana na madai ya Israel ya kutaka kutambuliwa kama ni taifa la Kiyahudi na kuhusu makaazi ya walowezi wa Kiyahudi yaliojengwa katika ardhi ya Wapalestina inayokaliwa kwa mabavu na Israel ambapo Wapalestina wanataka kuunda taifa lao.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Picha: Brendan Smialowski/AFP/Getty Images

Kuhusiana na suala la kusaini mikataba ya kimataifa wiki iliopita Wapalestina wamesema huo ulikuwa ni utaratibu wa kawaida baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hapo mwaka 2012, kutambuwa kuwa ni ukweli wa mambo kwamba kuna taifa la Palestina .

Waziri Mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu katika mkutano wa baraza la mawaziri hapo jana aliahidi kuchukuwa hatua za kulipiza kisasi ambazo hakuzifafanua kufuatia kusainiwa kwa mikataba hiyo.

Madai ya Wapalestina

Afisa mwandamizi katika chama cha Fatah cha Rais Mahmud Abbas wa Mamlaka ya Wapalestina amesema Wapalestina wanataka ahadi ya maandishi kutoka serikali ya Netanyahu yenye kulitambuwa taifa la Palestina katika ardhi yote ya Ukingo wa Magharibi na ambayo Israel iliiteka katika Vita vya Mashariki ya Kati mwaka 1967 na Jerusalem ya Mashariki ukiwa ndio mji mkuu wake.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas.Picha: Reuters

Israel imeielezea mipaka hiyo ya Ukingo wa Magharibi kuwa hailindiki na inaichukulia Jerusalem ya Mashariki kama sehemu ya mji mkuu wake madai ambayo hayatambuliwi kimataifa. Israel ilijitowa kwenye Ukanda wa Gaza ambao hivi sasa unatawaliwa na kundi la Hamas hapo mwaka 2005.

Wapalestina pia wanadai kusitishwa kwa shughuli za ujenzi katika makaazi ya walowezi wa Kiyahudi na kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina.

Wiki iliopita waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameelezea kukatishwa tamaa na pande hizo mbili na kusema kwamba Marekani inatathmini upya iwapo iendele na dhima yake ya upatanishi katika mazungumzo hayo.

Mwandishi: Mohamed Dahman/ Reuters/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman