1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Hatua za Afrika dhidi ya Covid-19 zatishia uchumi

Iddi Ssessanga
25 Machi 2020

Mataifa ya Afrika yametangaza amri za kutotoka nje katika juhudi za kudhibiti mripuko wa covid-19, na kuzusha hofu ya machafuko kwa wafanyakazi wa vipato vya chini na serikali zenye uhaba wa fedha na mizigo ya madeni.

https://p.dw.com/p/3a0oZ
Südafrika Kapstadt | Coronavirus | Busbahnhof
Picha: Reuters/M. Hutchings

Visa vya maambukizi ya virusi vya corona vimeongezeka barani Afrika katika muda wa wiki iliyopita hadi kufikia jumla ya 2,137 na vifo 62, kwa mujibu wa hesabu za shirika la habari la Ufaransa AFP, na kuyalazimu mataifa kuchua hatua kali za kukabiliana na janga hilo.

Afrika Kusini, taifa lenye uchumi ulioendelea zaidi barani Afrika -- ambalo kwa visa 554 lina mripuko mkubwa zaidi -- siku ya Jumatatu ilitangaza vikwazo vya nchi nzima.

"Bila hatua thabiti, idadi ya watu walioathirika itaongezeka haraka -- hadi kufikia mamia kwa maelfu," alisema rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wakati akitangaza marufuku ya kutotoka nje bila sababu za msingi.

Kuna hofu kwamba miundombinu dhaifu ya kiafya barani Afrika italiacha bara hilo hatarini kushambuliwa vibaya na mripuko huo kwa kiwango kinachoshuhudiwa barani Ulaya.

Mataifa mengine yanafuata kwa hatua sawa na hizo. Zaidi yanatazamiwa kutangaza katika siku zikazo. Jumatatu Senegal, Cote di'Voire zote zilitangaza hali za dharura na kuamuru watu wasitembee usiku.

Südafrika Hillcrest | Coronavirus | Kauf von Toilettenpapier
Kufuatia kutangazwa kwa vizuwizi nchini Afrika Kusini, watu walikimbilia kufanya manunuzi ya pupa.Picha: Reuters/R. Ward

Cote di'Voire siku ya Jumanne ilisema imerikodi jumla ya visa 73 na ingeyazuwia maeneo hatua kwa hatua, kutegemeana na namna virusi hivyo vinavyosambaa. Senegal imerekodi visa 86 vya virusi vya corona mpaka sasa, ilisema wizara yake ya afya siku ya Jumanne.

Katika ishara ya kuongezeka kwa mambukizi ya virusi corona, waziri mkuu wa Cote di'Voire Anadou Gon Coulibaly alisema kwenye ukurasa wa Twitter kwamba alikuwa amejiweka kwenye karantini baada ya kutangamana na mtu alieambukizwa.

Kitisho cha kusambaratika uchumi wa Afrika

Wakati virusi hivyo vikisambaa, kuna hofu pia kwamba mataifa maskini na yalio na mzigo mkubwa wa madeni yatashindwa kuchukuwa hatua stahiki.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Jumanne aliwaomba viongozi wa mataifa ya kundi la G7 kutoa kiasi cha dola bilioni 150 katika ufadhili wa dharura ili kushughulikia mripuko wa virusi vya corona, akisema "unatishia kuusambaratisha uchumi wa mataifa ya Afrika."

Aliongeza kuwa wakopeshaji wanapaswa kufuta sehemu ya madeni ya mataifa kwa mataifa yenye kipato cha chini. Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian aliliambia bunge la Ufaransa Jumanne kuwa kutakuwa na mpango wa ufadhili wa kifedha wa Ulaya kwa ajili ya mataifa maskini yanayopambana dhidi ya virusi hivyo.

"Nafikiria hasa juu ya Afrika," alisema.

Utekelezaji wa marufuku za kutoka na kujitenga kijamii katika mataifa maskini pia unasababisha wasiwasi wa kiuchumi kwa ngazi ya ndani. Kaya mara nyingi zina watu wengi, na wafanyakazi katika uchumi usio rasmi hawawezi kujitenga wenyewe nyumbani bila kutelekeza majukumu yao ya kimaisha.

Matshidiso Moeti, mkurugenzi wa kanda wa shirika la afya duniani WHO barani Afrika, alikiri kuhusu ugumu huu katika mkutano na waandishi wa habari wili iliyopita.

Symbolbild Hände waschen
Watu wanahimizwa kunawa mikono kila mara ili kuzuwia kuenea kwa virusi vya corona.Picha: Imago Images/M. Westermann

Alisema hatua kama hizo zilikuwa "changamoto kubwa"  na kwamba WHO ilikuwa inafanyia kazi mikakati mingine kama vile kuhakikisha vitakatishaji vinapatika kwa wingi.  Wenyeji wanazidi kutiwa wasiwasi wakati ambapo hatua za udhibiti barani humo zinazidi kuumiza.

"Wanafunga vibanda, mikahawa, lakini vipi tutaweza kuhudumia familia zetu?" aliuliza Nemy Fery, anaeendesha kibanda cha chakula mjini Abidjan, mji mkubwa wa Cote di'Voire. Aliongeza kuwa atajaribu kuuza vyakula vya kuondoka navyo -- na kutafuta kazi nyingine.     

Kuna wasiwasi sawa na huo katika taifa la Senegal lenye Waislamu wengi, ambako mamlaka zilikuwa tayari zinapambana wiki iliyopita kutekeleza marufuku ya kuswali misikitini.

Sabah Amar, mfanyakazi wa duka la zawadi, alisema watu wa Senegal "watakufa kwa njaa" kabla ya kufa kwa virusi vya corona. Watu kadhaa waliohijiwa na AFP mjini Dakar hata hivyo walisema wanaunga mkono hatua za serikali dhidi ya virusi vya corona.

"Napendelea kila kitu kifungwe. Hatuuzi chochote hivi sasa," alisema Amar. "Vinginevyo sote tunakwenda kufa."

Hatua za udhibiti na hofu ya walalahoi

Kaskazini mwa bara, waziri mkuu wa Misri Mostafa Madhouli siku ya Jumanne alitangaza amri ya kutotembea usiku.

Na mashariki mwa bara, Rwanda imeripoti kuongezeka maradufu kwa visa na kufikia 36, huku Sudan Kusini ikifunga mipaka yake ya angani na ardhini, isipokuwa tu kwa ugavi wa chakula na mafuta.

Südafrika l 25 Jahre Demokratie - Ende der Apartheid l Präsident Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.Picha: Getty Images/AFP/M. Spatari

Taifa la kisiwa la Cape Verde siku ya Jumanne lilitangaza kifo chake cha kwanza kutokana na virusi hivyo baada ya mtalii wa Kiingereza mwenye umri wa miaka 62 kufariki huko.

Cameroon pia ilirekodi kifo chake cha kwanza -- mwanaume alieambukizwa ugonjwa huo nchini Italia na kukutwa na Covid-19 Machi 14, kwa mujibu wa waziri wa afya Mananchi Manaouda.

Watu wanne wamefariki nchini Burkina Faso, ambayo ndiyo imeathirika zaidi katika kanda ya Afrika Magharibi ikiwa na visa 115 vilivyothibitishwa. Mataifa yaliotangaza hatua kali za kuzuwia yanatumia jeshi kutekeleza hatua hizo.

Doria za kijeshi nchini Senegal zitahakikisha watu wanaheshimu amri ya kutotembea usiku, kwa mfano. Ris wa Afrika Kusini pia alisema jeshi litatumika kutekeleza marufuku ya kutotoka nchini mwake.

Nombulelo Tyokolo, mwenye umri wa miaka 41, mfanyakazi wa ndani mjini Cape Town, ambaye analala chumba kimoja na mtoto wake, aliliambia shirika la AFP kwamba ana wasiwasi juu ya namna vizuwizi hivyo vitakavyofanya kazi.

"Nina hofu na wasiwasi kuhusu kukaa ndani kwa siku 21," alisema. "Tunapaswa kuchota maji nje na kwenda  chooni. Eeh Mungu tuhurumie."

Chanzo: AFP