1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za amani Mashariki ya Kati

Oumilkher Hamidou15 Septemba 2009

Mjumbe maalum wa Marekani George Mitchell azungumza na waziri mkuu wa Israel

https://p.dw.com/p/Jh7G
Waziri mkuu Netanyahu akutana na mjumbe wa Marekani G.MitchellPicha: AP

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na mjumbe maalum wa Marekani,George Mitchell wamekutana kwa lengo la kusaka maridhiano katika suala la ujenzi wa makaazi mepya ya wayahudi-kizingiti kikubwa cha kuanzishwa upya mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palastina.Mazungumzo yao yanatazamiwa kuendelea tena kesho.

Mazungumzo yao ya leo yamedumu saa tatu.Wanasiasa hao wawili wanapanga kukutana tena kesho asubuhi.Habari hizo zimetangazwa na ofisi ya waziri mkuu wa Israel.

Mwanzoni mwa mazungumzo yao,mjumbe maalum wa Marekani,George Mitchell alielezea matumaini "ya kuingia katika awamu hii mpya ya mazungumzo ili kufikia hatua itakayo wawezesha kusonga mbele haraka katika juhudi za kusaka amani" katika eneo hilo.

Mjumbe huyo maalum wa Marekani katika Mashariki ya kati,aliyeanza ziara yake hii mpya jumapili iliyopita,amepangiwa kukutana na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina,Mahmoud Abbas,leo usiku mjini Ramallah.

Hivi karibuni bwana Mitchell alisema "Marekani na Israel "wana hisia za aina moja" linapohusika suala la umuhimu wa kufufuliwa mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palastina hadi ifikapo mwisho wa mwezi huu.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel,bwana Mitchell anajaribu kusaka ufumbuzi wa suala tete la ujenzi wa makaazi ya wahamiaji wa kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi na Mashariki ya Jerusalem ili kurahisha mazungumzo kati ya kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmud Abbas na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu,chini ya upatanishi wa rais Barack Obama.Mazungumzo hayo yanaweza kufanyika pembezoni mwa mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa mataifa mjini New-York.

Akiwakaribisha mabalozi wa kigeni kuadhimisha mwaka mpya wa kiyahudi,rais shimon Peres amesema "hadhara kuu ya Umoja wa mataifa ni fursa nzuri ya kufufua utaratibu wa amani.

Suala watu wanalojiuliza ni kama waziri mkuu Netanyahu atakubali kweli kusitisha ujenzi wa makaazi mepya ya wayahudi.Leo asubuhi mbunge Ofir Akounis,ambae ni mkaribu wa waziri mkuu huyo aliiambia Radio ya kijeshi ya Israel tunanukuu:"masharti bado hayajafikiwa kuanza upya mazungumzo ya amani pamoja na wapalastina.

Mwandishi:Oummilkheir Hamidou/AFP

Mhariri:M.Abdul-Rahman