1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kidiplomasia kuhusu Syria zapamba moto

11 Julai 2012

Mpatanishi wa kimataifa katika mgogoro wa Syria Kofi Annan atalihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya hatua iliyopigwa kujaribu kusitisha ghasia nchini Syria. Urusi nayo imewaalika wapinzani wa Syria.

https://p.dw.com/p/15VB0
Juhudi za kidiplomasia juu ya mgogoro wa Syria zinaendelea
Juhudi za kidiplomasia juu ya mgogoro wa Syria zinaendeleaPicha: Reuters

Juhudi za kidiplomasia zinaendelea leo kutafuta ufumbuzi katika mgogoro waumwagaji damu nchini Syria. Kofi Annan atalihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, siku moja baada ya kukamilisha ziara iliyomfikisha katika miji mikuu ya Syria, Iran na Iraq. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara yake mjini Baghdad jana, bwana Annan alisema anao uhakika baraza la usalama litachukua hatua muafaka, hususan juu ya majukumu ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, ambao mudao wao utamalizika tarehe 21 mwezi huu wa Julai.

Kofi Annan alisema kwamba viongozi aliokutana nao katika ziara yake waliuunga mkono mpango wake wenye vipengele sita na ambao unalenga kumaliza ghasia nchini Syria kupitia njia ya mazungumzo.

Baada ya mazungumzo yake na rais wa Syria Bashar al Assad mjini Damascus, Kofi Annan alisema walikubaliana juu ya mpango mpya wa kumaliza mgogoro wa miezi 16, lakini hakueleza zaidi juu ya mpango huo, akisema anataka kwanza kuuwasilisha kwa viongozi wa kambi ya upinzani.

Upinzani waelekea Moscow

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov atawapokea wapinzani wa Syria
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov atawapokea wapinzani wa SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Kambi hiyo ya upinzani wa Syria leo hii pia iko mjini Moscow, kwa mwaliko wa serikali ya Urusi ambayo ni mshirika wa Rais Bashar ala Assad. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Lavrov atampokea Abdel Basset Sayda, kiongozi wa baraza la kitaifa la Syria, SNC, ambalo linayaleta pamoja makundi ya upinzani nchini Syria na ambalo linaungwa mkono wazi wazi na nchi za magharibi pamoja na baadhi ya mataifa ya kiarabu.

Urusi ni mshirika mkubwa wa serikali ya rais Bashar al-Assad, lakini imekanusha kuegemea upande wowote katika mgogoro unaoendelea nchini Syria. Naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Michael Bogdanov amesema kwao kipaumbele si mtu binafsi, na wanachotaka kukifanya ni kuzungumza na upinzani wa Syria juu ya hali halisi na inayotekelezeka katika juhudi za kumaliza umwagaji damu nchini mwao.

Lakini, kama anavyosema Fjodor Lukjanov, mhariri mkuu wa Jarida linalochambua nafasi ya Urusi katika siasa Ulimwengu, mkutano huu unaihusu Syria na Urusi yenyewe.

''Ni kuhusu Syria, hilo ni sahihi, lakini uhusiano baina ya Urusi na Syria unajumuisha mambo mengi, na mkutano huu utakuwa unahusu pia ushawishi wa Urusi katika siasa za kimataifa.'' Alisema Lukjanov

Upinzani Syria hautaki mvutano na Urusi

Abdel Basset Sayda, mwakilishi wa upinzani wa Syria
Abdel Basset Sayda, mwakilishi wa upinzani wa SyriaPicha: picture alliance / dpa

Upinzani wa Syria kwa upande wake unasema unakwenda Moscow ukiwa na azma ya kutumia busara kuifanya Urusi ielewe jinsi hali ilivyokuwa ikiendelea kuharibika, badala kuwapelekea wanadiplomasia wakuu wa nchi hiyo mlolongo wa malalamiko.

Msemaji wa baraza la kitaifa la Syria Bassma Kodmani, amesema ni nchi muhimu kwa Syria, ambayo wana imani kuwa inaweza kusaidia kugeuza ukurasa mpya katika uongozi wa Syria.

Wakati huo huo, Urusi imewasilisha kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, pendekezo la azimio jipya, ambalo linataka kurefushwa kwa ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, bila kitisho chochote cha vikwazo. Wanadiplomasia wamesema kuwa pendekezo hilo la Urusi linaweza kuwa hatua ya kwanza ya mivutano mikubwa katika baraza hilo, katika kuamua mustakabali wa ujumbe wa waangalizi hao, ambao muda wake wa sasa utamalizika tarehe 20 mwezi huu wa Julai.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman