1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za Kidiplomasia kusaka Ufumbuzi wa amani Ukraine

Oumilkher Hamidou5 Machi 2014

Wawakilishi wa Marekani na Urusi wanakutana kupunguza mvutano kuhusu mzozo wa Ukraine katika wakati ambapo nchi za Magharibi zinaishawishi Moscow iwarejeshe wanajeshi wake kambini huko Crimea

https://p.dw.com/p/1BKUn
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry akiwasha mshumaa alipoweka shada la mawardi katika uwanja wa Maidan mjini KievPicha: Reuters

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, John Kerry, na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, watakutana ana kwa ana kwa mara ya kwanza hii leo tangu mzozo wa Ukraine uliporipuka, baada ya mkutano utakaohudhuriwa na wanachama wote watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini Paris.

Kabla ya mkutano huo, waziri John Kerry alisema:"Demokrasia na kuheshimiwa milki ya nchi na sio uamuzi wa upande mmoja wa kutumia nguvu, ndivyo vitakavyosawazisha mvutano kama huu katika karne ya 21. "Rais Barack Obama na mimi binafsi tunataka kuiambia wazi kabisa Urusi na ulimwengu kwa jumla, sisi hatutafuti malumbano, kuna njia bora zaidi kwa Urusi kutetea masilahi yake ya haki nchini Ukraine."

Juhudi za kidemokrasia zimeshika kasi

Wakati huo huo, wawakilishi wa Jumuia ya Kujihami ya NATO na wale wa Urusi watakuwa pia na mazungumzo mjini Brussels kuepusha mvutano kati ya wanajeshi wa Urusi na wale wa Ukraine katika jimbo la Crimea usije ukasababisha matumizi ya nguvu au kuiona Moscow ikiingia pia katika sehemu ya mashariki ya Ukraine. Habari za hivi punde zinasema vikosi vya Urusi vimekidhibiti kituo cha kurushia makombora ya Ukraine katika Ghuba ya Crimea.

Ukraine Russland Krim Bildergalerie aus Sevastopol
Wanajeshi wa Urusi wakipiga doria huko CrimeaPicha: DW/F. Warwick

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, amesema viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaokutana kesho mjini Brussels wataamua kama Urusi iwekewe vikwazo, ikiwa hadi wakati huo hali ya mambo haijatulia.

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Ufaransa, BFM, Laurent Fabius alisema wawakilishi kutoka pande zote zinazohusika na mzozo wa Ukraine wamepania kusaka ufumbuzi wa kisiasa kuhusu mzozo huo.

Mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, amesisitiza wakati wa mazungumzo pamoja na Mkuu wa Siasa ya Nje ya Umoja wa Ulaya, Bibi Catherine Ashton, kwamba makubaliano yaliyofikiwa Februari 21 iliyopita kati ya Rais Viktor Yanukovich na upande wa upinzani ndio yanayostahiki kutumika kama msingi wa kurejesha utulivu nchini Ukraine.

Bibi Ashton ameamua kuakhirisha ziara yake mjini Kiev hii leo kwa sababu ya mikutano inayofanyika Brussels na Paris.

Rais wa Uchina azungumza na mwenzake wa Urusi

Na kwa mara ya kwanza tangu mzozo wa Crimea uliporipuka,Jamhuri ya Umma wa China imeacha kukaa kimya. Rais Xi-Jinping amezungumza kwa simu na kiongozi mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, na kusema baadaye Urusi inaweza kushirikiana na mataifa mengineyo ili kusaka ufumbuzi wa amani utakaosaidia kuleta utulivu katika eneo hilo na ulimwenguni kwa jumla.

Wladimir Putin Pressekonferenz 4.3.14
Rais Vladimir Putin wa UrusiPicha: Reuters

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reures/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef