1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kuwahamisha watu kutoka Afghanistan zashika kasi

Daniel Gakuba
18 Agosti 2021

Kampeni kubwa ya kimataifa inaendelea kuwahamisha raia wa kigeni na wa Afghanistan waliofanya nao kazi, wakati maelfu ya watu waliojawa na hofu ya utawala wa Taliban wakizidi kufurika katika uwanja wa ndege wa Kabul.

https://p.dw.com/p/3z6Yf
Bundeswehr bereitet Evakuierung von Deutschen in Afghanistan vor
Picha: Moritz Frankenberg/dpa/picture alliance

Baada ya mkutano wa nchi wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO hapo jana, katibu mkuu wa Jumuiya hiyo, Jens Stoltenberg alisema kuwa ndege zaidi zitapelekwa Kabul kusaidia shughuli hiyo, ambayo ilikwamishwa na mtafaruku uliotokea Jumatatu.

Soma zaidi:  Umoja wa Mataifa wataka ulimwengu kuisaidia Afghanistan

Pamoja na ndege hizo Marekani pia imepeleka wanajeshi 1000 wa ziada na kufikisha maafisa 4000 wanaosimamia kazi hiyo ya kuwahamisha watu. Msemaji wa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, Steffen Seibert amesema kuwa Kansela huyo amefikia makubaliano na viongozi wa Ufaransa, Uingereza na Italia, kushirikiana katika operesheni hiyo ya kuwaondoa raia wao kutoka Afghanistan.

Wizara ya ulinzi ya Ujerumani imesema tayari ndege za nchi hiyo zimewahamisha watu 260 kutoka Afghanistan.

Ulaya kushirikiana katika kuwaweka salama raia wao walioko Afghanistan

Suala hilo la kuwaondoa raia wa kigeni kutoka Afghanistan lilikuwa agenda kuu kwenye mkutano kati ya mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell na mawaziri wa nchi za nje wa Umoja wa Ulaya, ambao ulifanyika jana jioni kwa njia ya video.

Brüssel | Sondertreffen der EU-Außenminister | Konflikt in Afghanistan
Mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya na mawaziri wa nje wa umoja huo katika mkutano kuhusu hali nchini AfghanistanPicha: Johanna GeronReuters/AP/dpa/picture alliance

Akizungumza baada ya mkutano huo, Borrell alisema azimio muhimu lililofikiwa ni kufanya kila juhudu kuhakikisha kuwa raia wa nchi za Ulaya walioko nchini Afghanistan wanaondolewa kwa njia salama na katika mazingira mazuri.

Soma zaidi:  Ndege za kijeshi zarejelea safari zake Kabul

Azimio hilo pia linawahusu Waafghanistan waliofanya kazi na Umoja wa Ulaya katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, ikiwa watapenda kuondoka nchini mwao.

Umoja wa Ulaya kuzungumza na Wataliban

Kama ilivyokwishadhihirika kutoka pande nyingine zenye ushawishi duniani kama Urusi na China, Borrell amesema Ulaya pia haitakuwa na chaguo jingine isipokuwa kuzungumza na Wataliban, kwa sababu wameshinda vita.

Hata hivyo, hali ya vurugu katika uwanja wa ndege mjini Kabul imekuwa changamoto kubwa kwa shughuli hiyo ya kuwahamisha raia wa kigeni. Jana jioni ndege ya Ujerumani iliweza kuwachukua watu 125 kutoka Afghanistan, kufuatia ukosoaji mkubwa baada ya ndege ya kwanza kuondoka na wasafiri saba tu Jumatatu usiku.

Afghanistan Kabul Flughafen Evakuierung
Raia wa Afghanistan wanaohofu utawala wa Taliban wakisubiri nje ya uwanja wa Kabul, fursa ya kuondolewa nchini humo.Picha: AP Photo/picture alliance

Omid Nouripour, mtaalamu wa sera za nje kutoka chama cha walinzi wa mazingira-The Green cha hapa Ujerumani, aliiambia DW katika mahojiano kuwa mvurugano huo umeonyesha kuwa serikali ya Ujerumani haijajipanga vyema kukabiliana na hali ya Afghanistan kama ilivyoahidi.

Soma zaidi: Uturuki yafanya mazungumzo na pande zote Afghanistan

Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Florence Parly amezungumzia pia ugumu wa juhudi za kuwaondoa raia wa nchi yake kutoka Kabul, akisema tatizo kubwa ni namna ya wa kuwafikisha watu katika uwanja wa ndege wa mji huo mkuu.

Amesema kwa wakati huu Ufaransa inategemea ulinzi wa Marekani katika uwanja huo, na kwamba idadi ya Wafaransa watakaoondolea itategemea nafasi watakayopewa ndege zao kutua kwenye uwanja wa Kabul.

Taliban yaahidi kuheshimu haki za binadamu, chini ya sheria za kiislamu

Huku haya yakiarifiwa, jioni ya jana msemaji wa Taliban, Zubihullah Mujahid alifanya mkutano na waandishi wa habari, wa kwanza tangu kundi hilo la itikadi kali za kiislamu kuukamata mku mji mkuu wa Afghanistan.

Afghanistan PK der Taliban | Zabihullah Mujahid
Msemaji wa Wataliban, Zabihullah Mujahid katika mkutano na waandishi wa habari mjini KabulPicha: Rahmat Gul/AP Photo/picture alliance

Katika sauti iliyotulia, alisema haki za raia wote wa Afghanistan, wakiwemo wanawake, zitalindwa kwa mujibu wa sheria ya kiislamu. Aliwataka Waafghanistan wote, hata wale waliofanya kazi na nchi za kigeni kubakia nchini mwao na kuchangia kuijenga.

Msemaji huyo alirudia mara kwa mara, kauli yake kuwa kila kitu kitakuwa katika misingi ya sheria ya kiislamu, ikiwemo sekta ya habari.

Zubihullah Mujahid amesema anazihakikishia nchi zote, na hasa Marekani, kuwa Afghanistan haitaruhusu makundi yoyote kutumia ardhi yake kuhujumu usalama wa nchi nyingine.

Awali, katibu mkuu wa umoja wa kujihami wa NATO, Jens Stoltenberg, alikuwa amewaonya Wataliban, kuwa ingawa vikosi vya jumuiya hiyo vimeondoka, bado vinao uwezo wa kuvishambulia vikundi vyote vya kigaidi vitakavyoweka makaazi yao nchini Afghanistan.

dpae, rtre, afpe