1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Juhudi za kupambana na ujambazi Kenya

Wakio Mbogho7 Machi 2024

Maafa na mashambulizi yanaendelea kushuhudiwa kwenye kaunti sita nchini Kenya, maeneo ambapo oparesheni ya kuwaangamiza majambazi inaendelea. Serijkali sasa inaweka mikakati kukabiliana na tatizo hilo.

https://p.dw.com/p/4dGoB
Jamii za wafungaji zinakumbwa na ukosefu wa usalama
Matukio ya wizi wa mivugo Kenya miongoni mwa jamii za wafugaji Kenya yamekithiriPicha: Reuters/G. Tomasevic

Kati ya mikakati ambayo Kenya inalenga kutumia ili kusitisha uovu huo ni kubuni shule za malazi zitakazowachukua wanafunzi kutoka jamii hasimu. 

Hofu imeendelea kutanda kufuatia visa viwili vya uvamizi wa punde zaidi kufanyika eneo la Samburuambapo watu wawili walifariki baada ya majambazi kuwavamia na kuiba mifugo. 

"Wamemuuwa ndugu yangu mkubwa, alikuwa polisi mstaafu, alikuwa anachunga ng'ombe zake tu. Tumepoteza tena watu wengine wawili, hatuwezi kufikiri kwa nini serikali haitusaidii. Tunawalilia kila siku, tunataka amani."

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki ametangaza kwamba uhalifu wa wizi wa mifugo umeorodheshwa kama aina ya ugaidi. Mashambulizi na mauaji ya mara kwa mara baina ya jamii yamepelekea serikali ya Kenyakuendesha operesheni ya kuutokomeza uhalifukatika kaunti sita za Samburu, Baringo, Elgeyo Marakwet, Turkana, Pokot Magharibi, na Laikipia.

Waziri Kindiki ametangaza kuwa maafisa maalum wa usalama wametumwa katika maeneo hayo sita kuwakabili viongozi wa majambazi hao. "Jinsi maafisa maalum wametusaidia kupambana na magaidi, suluhisho la hawa majambazi sugu, wale makamanda wakali, tutawatumia hao maafisa maalum wa usalama."

Kijana kutoka jamii ya Orma
Serikali inakabiliwa na changamoto ya kuyakabili machafuko yanasobabishwa na majambazi wanaoiba mifugoPicha: imago images/Nature Picture Library

Pamoja na hayo, wizara ya usalama wa ndani inaweka mikakati ya kujenga shule tano za malazi kwenye maeneo hayo. Shule hizo zitawachukua watoto kutoka jamii hasimu ambao wataishi na kusoma pamoja. Waziri anasema hatua hii itasaidia kuangazia kiini cha ujambazi huo unaosababishwa na mila na itikadi za jamii zilizoko maeneo hayo. "Hakuna mtoto ambaye huzaliwa jambazi. Shule moja itakuwa upande mmoja wa mpaka wa eneo la Tiaty, na shule nyingine itakuwa upande wa Elgeyo Marakwet. Na lazima Watoto kutoka jamii zote hasimu wawe katika kila shule. Tutaka kujitosa katika shughuli za kujenga amani. Na sasa tutawajumuisha wadau wengine.”

Huku hayo yakijiri, viongozi kadhaa wakiwemo magavana, wabunge na madiwani kutoka maeneo hayo sita yenye utata wanalalamika kutumiwa miito ya mara kwa mara kufika kwenye idara ya upelelezi kwa ajili ya uchunguzi ilhali hakuna hatua zinazochukuliwa.

Gavana wa Samburu Jonathan Lelelit aliyefika mbele ya kitengo cha jinai na upelelezi eneo la Bonde la Ufa kwa mara ya pili chini ya mwezi mmoja, kueleza anachokijua kuhusu ujambazi unaoendelea kwenye kaunti yake, amesema usumbufu huo hautaleta amani kwenye eneo hilo.  "Badala ya mkuu wa polisi na timu yake waende wakashughulikie watu wanaotuua, wanaanza kuwaita wanasiasa kuja kuandika taarifa. Mimi ni mwathiriwa, watu wangu ndio wanawauwa, mimi nije niandike taarifa kwamba tuko mazishi kesho? Mtu mwingine yuko kwenye chumba cha wafu? Hii ni aibu kwa nchi yetu ya Kenya."

Operesheni ya kumaliza uhalifu iliyoanza mwaka mmoja uliopita haijaonekana kufikia malengo yake, kwani mashambulizi na maafa yanaendelea kushuhudiwa.