1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zoezi la kubadilishana wafungwa

28 Machi 2016

Saud Arabia na waasi wa kishia wa Yemen wamebadilishana wafungwa kwa mara nyengine tena na kuthibitisha wakati huo huo azma ya kutuliza hali ya mambo kabla ya silaha kuwekwa chini na kuitishwa mazungumzo ya amani

https://p.dw.com/p/1IKmP
Waasi wa HouthiPicha: picture-alliance/AP Photo/H.Mohammed

Wasaudi tisa waliokuwa wakishikiliwa Yemen wameachiwa huku wayemen 109 waliokuwa wamekamatwa katika maeneo ya opereshini za kijeshi" wakikabidhiwa viongozi wa Yemen-habari hizo zimetangazwa na Ushirika unaoongozwa na Saudi Arabia.

Zoezi hilo la kubadilishana wafungwa,la pili la aina yake,limetokea jana-taarifa ya ushirika huo unaoongozwa na Saud Arabia imesema bila ya kutaja kama wasaudi hao waliokuwa wakishikiliwa Yemen ni wanajeshi au raia au kama wayemen ni wahuthi au la.

Zoezi la kwanza la kubadilishana wafungwa lilifanyika Marchi 9 iliyopita kufuatia juhudi za upatanishi za makundi ya kikabila juhudi zilizopelekea pia kuwekwa chini silaha kwasababu za kiutu katika eneo la mpakani kati ya Saud Arabia na Yemen.

Ushirika wa nchi za kiarabu waridhika na mpango wa kuweka chini silaha Yemen

Katika taarifa iliyotangazwa leo,ushirika unaoongozwa na Saud Arabia unasema umeridhika na kuendelea hali ya utulivu katika eneo hilo la mpakani na unataraji makubaliano ya kuweka chini silaha yataenea pia katika viwanja vya mapigano ili kurahisisha juhudi za kupeleka misaada ya kiutu kote nchini Yemen na kuuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa za kupatikana ufumbuzi wa kisiasa nchini Yemen kuambatana na azimio nambari 2216 la Baraza la usalama.

Jemen Sanaa Ruinen nach Bombenangriffen Kind
Magofu kufuatia mashambulio ya mabomu SanaaPicha: picture-alliance/dpa/Y. Arhab

Zoezi jipya la kubadilishana wafungwa limetokea baada ya kutangazwa mpango wa kuweka chini silaha kuanzia April 10 na kuanza upya siku nane baadae mazungumzo ya amani ya Yemen nchini Kuweit,yatakayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Saud Arabia yaashiria amwisho wa opereshini za kijeshi Yemen

Yemen,nchi masikini ya raasi ya baraarabu inagubikwa na vurugu tangu waasi wa Houthi walipoingia Sanaa septemba mwaka 2014.Saud Arabia inawatuhumiu waasi hao wa madhehebu ya shia kuwa na mafungamano na Iran.

Saudi-Arabien Ahmed Asiri
Jenerali Ahmed Asiri wa Ushirika unaoongozwa na Saud ArabiaPicha: picture-alliance/AP Photo/H. Jamali

Mzozo wa Yemen umepelekea watu zaidi ya 6200 kuuwawa na zaidi ya 30 elfu kujeruhiwa-kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa mataifa linalosema asili mia zaidi ya 80 ya wakaazi wa nchi hiyo wanahitaji msaada wa kiutu-wakiwemo zaidi ya wayemen milioni mbili na nusu walioyapa kisogo maskani yao.

Akizungumza na shirika la habari la AFP,Marchi 26 iliyopita, msemaji wa ushirika wa nchi za kiarabu unaoongozwa na Saud Arabia,jenerali Ahmed Assiri amezungumzia juu ya "kukurubia mwisho wa opereshini za kijeshi nchini Yemen.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga