1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za uokozi Mumbai

Thelma Mwadzaya28 Novemba 2008

Maafisa wa kijeshi nchini India wanaripotiwa kufyatuliana risasi na wapiganaji wa kiislamu katika eneo lililoshambuliwa kwa mabomu siku ya Jumatano

https://p.dw.com/p/G40U
Watalii nje ya hoteli ya Taj MahalPicha: AP

Taarifa zinaeleza kuwa wapiganaji hao bado wanaendelea kuwazuilia mateka wa kigeni kwenye jingo moja lililokaribu.Hali hiyo imetokea baada ya wapiganaji wa kundi la Deccan Mujahideen kushambulia hoteli mbili za kifahari kwenye eneo kuu la biashara mjini Mumbai.


Kwa mujibu wa kiongozi mmoja wa kikosi hicho cha makamanda wa kijeshi yapata maiti 15 zimeonekana kwenye chumba kimoja cha hoteli ya kifahari ya Taj Mahal.Idadi kamili ya maiti hizo inaripotiwa kufikia 50 mpaka sasa.Makamando hao walipata pesa,silaha na kitambulisho cha nchi ya Mauritius wanachoshuku kilikuwa cha mmoja wa wapiganaji hao aliyekuwa amejifinika uso kwa kitambara cheusi.


Kwa mujibu wa maafisa wa serikali na kijeshi operesheni nzima ya uokozi inatarajiwa kukamilika katika kipindi cha saa chache zijazo.Jumla ya watu 121 wanaripotiwa kuuawa katika mashambulio hayo.Waziri Mkuu wa India Manmohan Singh ameinyoshea kidole nchi jirani kwa kuhusika na mashambulio hayo.''Ni bayana kwamba kundi lililotekeleza mashambulizi hayo ambao si wenyeji wa nchi hii walikuwa na lengo maalum la kuvuruga mambo katika mji mkuu wa kibiashara humu nchini.Tutachukua hatua zote zile kuhakikisha kuwa vitendo vya kigaidi havitokei tena.''

Nchi jirani ya Pakistan nayo pia imelaani vitendo hivyo na kuahidi kutoa ushirikiano katika vita dhidi ya ugaidi.

Kwenye eneo jengine la tukio katika hoteli ya kifahari ya Trident-Oberoi wageni walionekana wakitoka nje na mizigo yao na kusindikizwa hadi kwenye mabasi yaliyokuwa yakiwasubiri.


Wageni hao walizuiliwa mateka kwa kipindi cha muda wa saa 36.Duru za polisi zianeleza kuwa jumla ya wageni 93 waliokolewa.

Mpiganaji mmoja bado anadhaniwa kuendelea kuwashikilia mateka wawili kwenye hoteli ya kifahari ya Taj Mahal ambayo pia ilishambuliwa.Luteni Jenerali N .Thamburaj aliwaelezea waandishi wa habari kuwa wengi ya wageni na wafanyikazi wa hoteli hiyo waliweza kuokolewa.

Mji wa Mumbhai ulio na wakazi milioni 18 ndio makao makuu ya kibiashara nchini India pamoja vilevile sehemu inayotengezwa filamu maarufu Bollywood.

India iliyo na idadi kubwa ya waumini wa dini ya KiHindi na idadi ndogo ya Waislamu imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi kwa miongo mingi.Mashambulio hayo ya juzi yanadhaniwa kuwa na lengo la kuwavunja moyo wawakezaji wa kigeni.


Kwa upande mwingine nchi ya Australia ilitangaza rasmi kuwa inawaonya raia wake kutozuru India kwasababu ya hofu ya ugaidi.

Soko la hisa nchini India limefunguliwa tena hii leo baada ya kufungwa hapo jana.Bei katika soko hilo zinaripotiwa kupungua kwa asilimia tano.


Yapata wapiganaji 25 waliojihami kwa bunduki na guruneti waliushambulia mji wa Mumbai siku ya jumatano na kulenga maeneo yanayotembelewa sana na watalii na wafanyabiashara.Shambulio hilo lilitokea pia kwenye hoteli za kifahari za Taj Mahal na Oberoi.Duru za polisi zinaeleza kuwa yapata wapiganaji 7 wameuawa mpaka sasa na washukiwa wengine tisa wamekamatwa.Polisi 12 nao pia waliuawa akiwemo mkuu wa kitengo cha kupambana na ugaidi nchini India.