1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za uokozi zinaendelea mjini Beirut

Admin.WagnerD5 Agosti 2020

Vikosi vya uokozi vimeendelea na juhudi za kuwatafuta wahanga kutoka vifusi vya majengo yaliyoporomoka siku moja tangu mlipuko mkubwa kwenye bandari ya mji mkuu wa Lebanon, Beirut, kusababisha vifo vya watu 100.

https://p.dw.com/p/3gRHb
Libanon | Gewaltige Explosion in Beirut: Mann wird evakuiert
Picha: Reuters/M. Azakir

Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Lebanon George Ketteneh ameliambia Shirika la Habari la Ujerumani, DPA, kuwa idadi ya vifo kutokana na mkasa huo inaweza kuongezeka katika wakati ambapo kiasi watu 4,000 wamejeruhiwa kwa kiwango tofauti.

Afisa mmoja wa vikosi vya usalama amesema bado wanaendelea kutafuta watu waliokwama chini ya mabaki na vifusi vya majengo hususani katika eneo la kuzunguka bandari ya Beirut ambako mlipuko ulitokea.

Mapema leo vikosi vya uokozi vilikuwa vikiondowa mabaki ya vitu ili kufungua barabara pamoja na kuanza matengenezo baada ya mlipuko wa jana kuharibu kwa sehemu kubwa majengo, magari na kuzusha taharuki kwa wakaazi wa mji wa Beirut.

Hadi sasa ripoti zinasema chanzo cha mripuko huo ni moto uliozuka katika ghala moja iliyohifadhi shehena ya fashifashi na kemikali hatari ya Amonium Nitrate ambayo ilikamatwa karibu miaka 6 iliyopita.

Waziri Mkuu Diab atoa ahadi ya kuchukua hatua

Libanon TV-Ansprache von Ministerpräsident Hassan Diab
Waziri Mkuu wa Hassan DiabPicha: AFP/DALATI AND NOHRA

Katika hotuba yake kwa taifa waziri mkuu wa Lebanon Hassan Diab ametoa wito kwa mataifa yote na marafiki wa nchi yake kutoa msaada kwa taifa hilo dogo akisema linashuhudia janga kubwa kutokana na maafa ya mkasa wa mjini Beirut.

Diab pia ameahidi kuchukua hatua kwa wote waliohusika na kutokea kwa janga hilo.

"Kilichotokea hakitopita bila uwajibikaji, wale wanaohusika watalipa kutokana na janga hili. Hii ni ahadi kwa waliopoteza maisha na waliojeruhiwa. Hii ni azma ya taifa, kutakuwa na ukweli uliotangazwa kuhusu ghala hatari ambalo limekuwepo tangu 2014, kwa miaka 6" amesisitiza Diab 

Mataifa mbalimbali duniani yameendelea kutuma salamu za pole na rambarambi kwa Lebanon huku mengi yakiahidi kutuma msaada wa uokozi na fedha kuisadia nchi hilo kupambana na maafa yaliyotokea.

Iran, Ufaransa, Ubelgiji, Jamhuri ya Czech, Uturuki na Uholanzi na Uingereza ni miongoni mwa mataifa yaliyosema yanatuma waokoaji na shehena za vifaa na vyakula kwenda mjini Beirut kuongeza juhudi za utafutaji wahanga na kuwasaidia waliojeruhiwa.

Israel pia imeomba kuruhusiwa kutoa msaada 

Libanon | Gewaltige Explosion in Beirut: Feuerwehr löscht Brand
Picha: Reuters/M. Azakir

Israel pia ambaye imekuwa kwenye mvutano na Lebanon imesema iko tayari kuwatibu majeruhi wa mlipuko wa mjini Beirut.

Mlipuko huo ambao ni mbaya kabisa katika historia ya taifa hilo la Mashariki ya Kati umetokea wakati Lebanon inakabiliwa na mzozo mkubwa wa kiuchumi kuwahi kushuhudiwa tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1975-1990.

Tayari rais Michel Aoun wa Lebanon ametangaza kuwa serikali itatoa dola milioni 66 kusaidia kupunguza athari za tukio hilo kwa taifa hilo ambalo mbali ya mzozo wa uchumi linazongwa pia na kadhia ya janga la virusi vya corona.

Mwandishi: Rashid Chilumba/DPA/Afp/Reuters

Mhariri: Gakuba, Daniel