1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya kimataifa yalaani vikali mashambulizi ya Algeria

12 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CaSS

ALGIERS:

Kundi lenye mahusiano na mtandao wa Al Qaeda limedai kuwa ndio lililohusika na miripuko miwili ya bomu katika mji mkuu wa Algeria,Algiers.Kundi hilo,katika mtandao wa Internet limesema,watu wawili waliojitolea maisha muhanga walifanya mashambulizi hayo.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Algeria imesema,watu 26 wameuawa na wengine 177 wamejeruhiwa,lakini kwa mujibu wa duru za hospitali,takriban watu 70 wamepoteza maisha yao katika miripuko hiyo miwili.

Wakati huo huo msemaji wa Umoja wa Mataifa amearifu kuwa wafanyakazi 11 wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa-UNHCR waliuawa katika mripuko mmojawapo.Mripuko huo uliteketeza sehemu ya jengo lililokuwa likitumiwa na UNHCR.Katika shambulizi la pili,basi lililojaa wanafunzi wa chuo kikuu liliripuliwa nje ya Mahakama Kuu.

Wakati huo huo,Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amelaani vikali mashambulizi ya Algeria.Amesema,ni jambo lisilokubalika katika hali yo yote ile na wala haliwezi kuhalalishwa kwa vyo vyote.

Mashambulizi hayo pia yamelaaniwa vikali na jumuiya ya kimataifa.