1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya za kimataifa zatofautiana matokeo ya uchaguzi Congo

Bruce Amani
10 Januari 2019

Hisia na maoni mbalimbali yanaendelea kutolewa kuhusiana na matokeo hayo ya uchaguzi wa rais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

https://p.dw.com/p/3BIen
DR Kongo Goma Lage nach Wahlsieg von Tshisekedi
Picha: Getty Images/AFP/A. Huguet

Ufarasa imeyapinga matokeo hayo ikisema kuwa ushindi uliotangazwa wa kiongozi wa upinzani Felix Tsisekedi hauendani na matokeo na kuwa mpinzani wake Martin Fayulu anaonekana kuwa ndiye aliyeshinda.

Katika matamshi yaliyotolewa saa chache baada ya matokeo ya awali kutangazwa, Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni Jean-Yves Le Drian alisema mpinzani wa Tsisekedi Fayulu, ambaye alitangazwa kupata nafasi ya pili, ndiye angetangazwa mshindi.

Le Drian amekiambia kituo cha televisheni cha Ufaransa CNews kuwa inaonekana matokeo yaliyotangazwa hayaendani na ukweli halisi. Amesema Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Congo – CENCO lenye nguvu kubwa, ambalo liliwatuma waangalizi karibu 40,000 katika maeneo mbalimbali kufuatilia uchaguzi huo, linajua nani hasa alishinda uchaguzi huo huku takwimu zao zikiashiria kuwa Fayulu ndiye aliyeshinda.

DR Kongo Lage nach Wahlsieg von Tshisekedi
Wafuasi wa Felix Tshisekedi wakishangiliaPicha: Reuters/B. Ratner

Wiki iliyopita, CENCO ilisema inafahamu matokeo ya uchaguzi huo wa Desemba 30 na kuiomba tume ya uchaguzi kutangaza matokeo kwa "kuzingatia ukweli na haki”.

Ijapokuwa halikumtaja mshindi, tangazo lake wiki iliyopita lilizusha shutuma kali kutoka kwa muungano wa vyama tawala.

Matokeo ya awali yalitangazwa mapema leo, yakimuweka Felix Antoine Tsisekedi Tshilombo kuwa mshindi atakayechukua nafasi ya Joseph Kabila ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa miaka 18.

Katika nchi ambayo haijawahi kukabidhi madaraka kwa njia ya Amani tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka wa 1960, Le Drian ametoa wito wa utulivu.

Nchi nyingine ambayo imeonyesha kuwa na mashaka na matokeo hayo ya uchaguzi wa rais nchini Congo ni Ubelgiji ambayo ni mkoloni wake wa zamani.

DR Kongo Lage nach Wahlsieg von Tshisekedi
Wafuasi wakishangilia huku ulinzi ukiimarishwaPicha: Reuters/B. Ratner

Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni Didier Reynders ameliambia shirika la utangazaji la Ubelgiji RTBF kuwa Ubelgiji itatumia kiti chake cha muda katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka ufafanuzi kuhusu ushindi wa kushangaza wa Felix Tsisekedi.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewaomba wadau wote katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kuepusha vurugu baada ya ushindi wa Tsisekedi.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephan Dujarric amewataka wadau kutumia taasisi zilizopo katika kutatua masuala yoyote ya uchaguzi huo kwa kuzingatia katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na sheria mwafaka za uchaguzi.

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Iddi Ssessanga