1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kabul. Taliban watishia kuwauwa mateka.

21 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBgd

Shirika la habari la AP linaripoti kuwa anayedhaniwa kuwa ni msemaji wa kundi la wapiganaji wa Taliban amesema kuwa Wajerumani wawili waliotekwa nyara watauwawa iwapo Ujerumani haitaondoa majeshi yake nchini Afghanistan. Wajerumani hao pamoja na wenzao watano raia wa Afghanistan walikuwa wanafanyakazi katika mradi wa bwawa la umeme wakati walipotekwa nyara siku ya Jumatano katika eneo la kati la jimbo la Wardak.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani , hata hivyo imeonyesha wasi wasi wake juu ya madai hayo kuwa Taliban inahusika na utekaji nyara huo.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Franz-Josef Jung pia amepuuzia madai hayo ya kuyaondoa majeshi ya Ujerumani.

Ujerumani inawanajeshi 3,000 kaskazini ya Afghanistan , kama sehemu ya jeshi la kimataifa la NATO.

Wakati huo huo serikali ya Afghanistan imesema kuwa wapiganaji wa Taliban wamewakamata raia 18 wa Korea pamoja na Waafghanistan watano waliokuwa katika basi kusini mwa jimbo la Ghazni nchini humo.