1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kambi za wakimbizi Berlin ya Magharibi

12 Agosti 2011

Ukuta wa Berlin ulijengwa takriban miaka 50 iliyopita. Kwa kujenga ukuta huo, serikali ya Ujerumani ya Mashariki, iliazimia kuzuia wimbi la wakimbizi kutoka eneo la jiji hilo ambalo halikuwa chini ya udhibiti wa Warusi.

https://p.dw.com/p/12FUb
Ukuta wa Berlin wakati huo.

Ukuta huo pia, ulimaanisha kumalizika enzi ya kambi nyingi kubwa za kuwapokea wakimbizi hao, upande wa magharibi wa jiji la Berlin. Kambi nyingi, zimefungwa na zimesahauliwa. Sasa, maonyesha maalum yanatoa fursa ya kutupia jicho kambi moja ya zamani na yanakumbusha hali ngumu iliyokuwepo. Mwandishi wetu Heiner Kiesel alietembelea maonyesho hayo, ameandika taarifa ifuatayo.

Kuna picha nyingi za watoto katika maonyesha hayo yaliyoitwa "Zimetoweka na Zimesahauliwa. Kambi za wakimbizi katika Berlin ya Magharibi". Picha hizo na hata mabango na chati zinazoeleza matukio ya wakati huo, zinaninginia katikakati ya chumba cha maonyesho. Picha zimechapishwa kwenye mashuka ya vitanda na mavazi na yameanikwa vizuri kwenye kamba ya nguo. Kwa mkuu wa maonyesho hayo, Enrico Heitzer, kamba hizo za nguo ni alama kuu ya maisha ya wakimbizi wa Kijerumani kambini. Ni alama ya kubakia muda mfupi kambini na mpango wa mpito, kwani watu hao waliishi eneo moja kwa muda mfupi kabla ya kuhamishwa kwenye kambi nyingine. Heitzer anaeleza.

Ausstellung Flüchtlingslager in Westberlin
Mwanahistoria Enrico HeitzerPicha: Heiner Kiesel

Hakujakuwepo mahala maalum pa kuweka nguo. Kamba zilizotumiwa kuning'iniza nguo, ndio zilizotoa fursa pia kujipatia mahala pa faragha."

Wageni wanaotembelea maonyesho hayo maalum katika kambi kuu ya dharura ya zamani ya Marienfelde, wanaona kuwa watu walikuwa wakibanana kambini. Mwanahistoria Heitzer anasema wimbi la wakimbizi lilipofikia kilele chake, hadi wakimbizi 20,000 walipaswa kupatiwa mahala pa kuishi katika Berlin ya Magharibi. Wakati wa vuguvugu la upinzani katika Ujerumani ya Mashariki (DDR) na kabla ya kujengwa ukuta wa Berlin, wengi walikimbilia upande wa Magharibi kwa kuvuka mipaka ya mji. Idadi ya wakimbizi iliambatana na matukio ya kisiasa katika DDR. Kwa mfano kati ya mwaka 1953 na 1961 kulikuwepo vituo 90 vya kuwapokea wakimbizi. Vituo vingine vilikuwa na watu 22 tu , lakini kulikuwepo maeneo mengi yaliyopokea maelfu ya watu. Mpaka kusambaratika kwa DDR katika mwaka 1990, kiasi ya wakimbizi milioni 1 na 35 elfu (1.35) walisambazwa katika majengo mbali mbali. Mkuu wa kituo cha makumbusho katika kambi kuu ya Marienfelde, Bettina Effner amesema walitembelea maeneo tofauti ya Berlin ya Magharibi ili kuweza kujua zaidi kuhusu kambi za wakati huo na kujionea jinsi wakimbizi walivyokuwa wakiishi. Wolf Rothe mwenye miaka 83 ni mmoja wao. Anasema mara nyingi hawakuwa na maji ya moto. Kwa kulinganisha na hivi sasa, chakula kilikuwa kibaya sana. Hata hivyo wakimbizi walifurahi kuwa upande wa Magharibi, hata kama hawakupokewa kama ndugu.Anaeleza hivi:

"Nani anaetaka kuwa na wakimbizi karibu yake. Watu walijifungia makwao kwa sababu mbali mbali. Ilidhaniwa wote walikuwa wakomunisti. Kulikuwepo hadithi za kila aina".

Rothe anasema, wakimbizi walipata shida kubwa kujijumuisha katika jamii mpya ya magharibi. Ukuta ulipojengwa miaka 50 iliyopita, idadi ya wakimbizi wa Kijerumani ilipungua sana. Kambi nyingi zikafungwa na zingine zikatumiwa kwa shughuli tofauti. Siku hizi wakimbizi na watu wanaomba hifadhi, wanaishi karibu na jengo la maonyesho huko Marienfelde. Wao pia wana matatizo yale yale kama watangulizi wao.

Mwandishi: Kiesel, Heiner/ZPR

Mhariri: Othman Miraji