1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni ya uchaguzi yatawala hivi sasa

17 Machi 2009

Nyongeza ya malipo ya uzeeni,umiliki wa silaha na serikali mpya inayoundwa nchini Israel ni baadhi ya mada zilizoshughulikiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo Jumanne.

https://p.dw.com/p/HE3a

Tukianza na gazeti la LANDESZEITUNG kutoka Lüneburg gazeti hilo linasema:

Wapokea pensheni ni raia wanaoweza kutegemewa kwenda kupiga kura wakati wa uchaguzi. Hilo si jipya. Kwa hivyo,wala haishangazi kuona kuwa serikali ya muungano safari hii imeshikamana na imekubali kuongeza malipo ya uzeeni katika mwaka huu wa uchaguzi, bila ya kuwa na mabishano yoyote. Yaonekana kuwa kampeni ya uchaguzi ndio inayotawala hivi sasa.

Gazeti la WESTFALLEN BLATT likiendelea na mada hiyo hiyo linauliza:

Je, ni bahati tu kuwa nyongeza kubwa kabisa ya pensheni kutokea tangu miaka 15 iliyopita huku magharibi ya Ujerumani imetangazwa miezi mitatu kabla ya kufanywa uchaguzi mkuu nchini humu? Vyo vyote vile, kila Euro na senti inafurahiwa na wastaafu. Lakini waelewe kuwa baada ya nyongeza ya tarehe mosi Julai, wastaafu watangojea miaka mingi kabla ya pensheni zao kuongezwa tena kwa kiwango cha asilimia 2.4 magharibi ya Ujerumani na asilimia 3.4 mashariki ya Ujerumani.

Tukitazama mada nyingine, gazeti la WETZLARER NEUE ZEITUNG linasema:

Serikali inayoundwa hivi sasa nchini Israel ni muungano ulio kizingiti kwa utaratibu wa amani.Sera imara za kutafuta suluhisho la amani zilizotangazwa na Rais wa Marekani, Barack Obama, zitapambana na sera kali zilizo kizuizi kwa mchakato wa amani. Maneno makali tu kutoka Ulaya na Marekani wala hayatosaidia kubadilisha msimamo wa muungano nchini Israel ulio kizuizi kwa amani. Itakuwa bora zaidi kushinikiza na kulazimisha, na hasa Netanyahu ashinikizwe kuukubali mchakato wa amani wa Annapolis unaotaka suluhisho la kuundwa taifa huru la Palestina.Tena, akubali bila ya kutoa masharti yo yote. Hatua hiyo ingetoa fursa ya kuundwa serikali ya muungano pamoja na Tzipi Livni.

Kufuatia mauaji yaliyosababishwa na kijana wa miaka 17 juma lililopita katika shule yake ya zamani kwa kutumia bastola ya baba yake, sauti zimepazwa kuhusu umiliki binafsi wa silaha. Gazeti la SÄCHSISCHE ZEITUNG linaeleza hivi:

Umma unataraji kuwa serikali sasa itachukua hatua fulani.Ni dhahiri kuwa baadhi kubwa ya wakaazi wana mashaka na Kansela anaesita-sita, kwani safari hii moja kwa moja,ameshauri ukaguzi mkali kuhusu umiliki wa silaha binafsi. Basi pendekezo la kufanywa ukaguzi wa ghafula katika nyumba za wamiliki silaha, bora litekelezwa haraka iwezekanavyo. Hata vilabu vya wasasi havitopinga hatua kama hiyo ili wenzao wanaokiuka utaratibu wa kumiliki silaha wapate kufichuliwa.

Mwandishi: P.Martin/ DPA

Muhariri: Miraji Othman