1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni zaanza tena Uingereza baada ya shambulizi

26 Mei 2017

Wanasiasa Uingereza wanarejea katika harakati za kampeni Ijumaa huku suala la usalama wa kitaifa likiwa juu kwenye ajenda, wakati ambapo polisi ya nchini humo iko mbioni kuuvunja mtandao wa kigaidi unaohusishwa na Libya.

https://p.dw.com/p/2dbQQ
	
Die Britische Premierministerin Theresa May
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Picture alliance/dpa/J. Taylor/PA Wire

Mtandao huo wa kigaidi unadhaniwa pia kuhusika na lile shambulizi la Manchester. Waziri Mkuu Theresa May na kiongozi wa chama cha Leba Jeremy Corbyn walikuwa wamesimamisha kampeni zao kufuatia shambulizi la Jumatatu katika tamasha la muziki lililowauwa watu 22, wakiwemo vijana wengi na kuwajeruhi wengine kiasi 62.

Wakati wa uzinduzi wa manifesto ya chama cha UK Independence UKIP, Alhamis, naibu kiongozi wa chama hicho kinachopinga uanachama wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya Suzanne Evans, alisema Waziri Mkuu May ni sharti achukue jukumu kwa shambulizi hilo la Manchester.

"Theresa May amewakubalia magaidi waliopigana katika kundi linalojiita Dola la Kiislamu kurejea tena nchini mwetu," alisema Suzanne. "Ameshindwa kuwazuia watu walio na itikadi kali kueneza chuki katika vyuo vyetu vikuu na misikiti. Chini ya uongozi wake, uhamiaji wa watu hata kutoka nje ya Umoja wa Ulaya umepindukia na uhamiaji kwa ujumla umevunja rekodi."

Uislamu wa itikadi kali ni saratani katika jamii ya Uingereza

Kiongozi wa UKIP Paul Nuttall aliyetoa wito wa hatua kuchukuliwa dhidi ya uhamiaji na kuimarishwa kwa usalama kufuatia lile shambulizi la Jumatatu, alisema wanasiasa Uingereza wamekuwa wadhaifu katika suala hilo kwa miaka mingi. Amemlaumu May kwa kudai kuwa amepunguza idadi ya maafisa wa polisi, walinzi wa mipaka na walinzi wa magereza.

UKIP-Mitgliederin Suzanne Evans
Naibu kiongozi wa UKIP Suzanne EvansPicha: picture alliance/empics/P. Toscano

"Nilishutumiwa na baadhi ya vyombo vya habari kwa kuuita Uislamu wa itikadi kali saratani katika jamii yetu, kufuatia shambulizi la Westminster," alisema Nuttal. "Siombi msamaha kwa kusema hivyo, na nitarudia leo, ni saratani inayohitaji kuondolewa."

Kiongozi wa upinzani Corbyn katika hotuba yake mjini London Ijumaa, anatarajiwa kusema ni jukumu la serikali kupunguza kitisho cha ugaidi kwa kuipatia polisi fedha wanazohitaji.

Chama cha kihafidhina kinaongoza kikiwa na asilimia 43

Kura ya maoni iliyofanywa na shirika la YouGov na ambayo matokeo yake yalitolewa Ijumaa, imewaweka Wahafidhina mbele wakiwa na asilimia 43 huku chama cha Leba kikiwa na asilimia 38, hii ikiwa ni afueni kubwa kwa chama hicho cha Leba kwani kura ya awali ilikuwa inaonesha chama cha Kihafidhina kilicho uongozini kiko kifua mbele kwa zaidi ya asilimia kumi.

Großbritannien Liverpool - Jeremy Corbyn nach Parteisieg
Kiongozi wa chama cha Leba Jeremy CorbynPicha: Reuters/P. Nicholls

YouGov katika uchunguzi wake iliwauliza maswali zaidi ya watu 2,052 siku ya Jumatano na jana Alhamis. Lakini wachambuzi wanasema Waziri Mkuu May aliyewahi kuhudumu kama waziri wa usalama wa ndani, huenda akanufaika katika uchaguzi kufuatia kubadilika kwa mtazamo huku uchaguzi mkuu ukikaribia.

"Iwapo usalama na ugaidi yatapewa kipau mbele, basi naona mshindi mmoja tu, Theresa May," alisema Steven Fielding, profesa wa siasa katika chuo kikuu cha Nottingham.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE

Mhariri: Josephat Charo