1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kanisa Katoliki lasikitishwa na unyanyasaji wa kingono

Grace Kabogo
13 Septemba 2018

Kanisa Katoliki limesema limefedheheshwa na kuabishwa kutokana na ripoti mpya ambayo inaonesha kuwa mapadri waliwanyanyasa kingono maelfu ya watoto nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/34ncY
Irland Referendum Homo-Ehe Katholische Kirche
Picha: picture alliance/empics/N. Carson

Ripoti hiyo iliyochapishwa na jarida la Spiegel pamoja na gazeti la kila wiki la Zeit, imeeleza kuwa mapadri 1,670 ambao ni sawa na asilimia 4.4 ya makasisi wa Kanisa Katoliki waliwanyanyasa watu 3,677 kati ya mwaka 1946 na 2014.

Kanisa Katoliki nchini Ujerumani liliagiza kufanyika kwa uchunguzi huo na ripoti hiyo ilikuwa iwasilishwe katika Baraza la Maaskofu Wakatoliki wa Ujerumani, DBK tarehe 25 ya mwezi huu wa Septemba. Ripoti hiyo imeeleza kuwa waathirika wengi walikuwa ni watoto wa kiume wenye umri mdogo na zaidi ya asilimia 50 walikuwa na chini ya umri wa miaka 13.

Madai ya ubakaji

Moja kati ya visa sita yanahusiana na madai ya ubakaji na robo tatu ya visa, waathirika na wahalifu walijuana kupitia kanisa. Askofu wa Jimbo la Trier, Mhashamu Stephan Ackermann ambaye pia ni msemaji wa DBK kuhusu unyanyasaji wa watoto, amesema ripoti hiyo imeliletea kanisa aibu. Amesema ripoti iliyochapishwa awali pia ilikuwa inasikitsha, hasa kwa sababu ripoti yote ilikuwa haijawafikia wajumbe wote wa DBK.

Irland | Besuch Papst Franziskus
Papa FrancisPicha: picture-alliance/dpa/empics/PA Wire/Y. Mok

Kwa mujibu wa watafiti wa uchunguzi huo, idadi kamili ya visa vya unyanyasaji huenda ikawa ya juu zaidi. Watafiti hao wamesema hawakuwa na uwezo wa kuyapata moja kwa moja mafaili kutoka katika rekodi za Kanisa. Badala yake, maafisa wa Kanisa waliyapitia kwanza mafaili muhimu yaliyohifadhiwa, kabla ya kuwakabidhi watafiti hao.

Likiwanukuu wachunguzi hao, gazeti la Zeit limesema katika baadhi ya visa palikuwa na ishara za wazi kwamba mafaili hayo yalibadilishwa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mafaili katika majimbo yapatayo mawili yaliharibiwa.

Chama cha mageuzi ya Kanisa Katoliki nchini Ujerumani kinachojulikana kama ''Sisi ni Kanisa'', kimesema kwamba ripoti hiyo inatia hasira, lakini huenda taarifa hiyo ni kidogo kuliko ile isiyojulikana.

Ripoti hiyo imefichuliwa wakati ambapo Kanisa Katoliki duniani limeandamwa na madai ya kashfa ya unyanyasaji wa kingono. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ameomba radhi na ameahidi kuwasaidia waathirika katika kuipata haki yao.

Aidha, jana Papa Francis alisema mwezi Februari ataandaa mkutano wa mabaraza ya maaskofu katika ngazi ya kitaifa ili kuzungumzia namna ya kukabiliana na kuzuia unyanyasaji wa kingono ndani ya Kanisa Katoliki.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA, Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef