1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vatican:Sheria mpya kuhusu unyanyasaji wa ngono yatangazwa

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
29 Machi 2019

Kuanzia sasa wafanyakazi wote katika makao makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican na wanadiplomasia wanaomwakilisha Papa duniani kote duniani wanatakiwa kutoa taarifa haraka juu ya madai ya unyanyasaji wa kingono

https://p.dw.com/p/3Fu09
Abschlussmesse der Versammlung "Jugendschutz in der Kirche" in der Regia-Halle im Vatikan
Picha: picture-alliance /Catholic Press Photo

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis ametangaza sheria mpya kuhusiana na unyanyasaji wa watoto kingono ndani ya taifa la Vatican. Mabadiliko hayo katika sera zake, Kanisa Katoliki linalenga kuwa mfano bora kwa waumini wa Kanisa hilo duniani kote.

Amri hiyo ya lazima, ingawa inaanzia padogo lakini inaashiria mwanzo wa sheria itakayowatumbukiza maafisa wa Kanisa Katoliki kwenye hatua za kisheria na hatimaye kukabiliwa na faini au kufungwa jela iwapo hawatatoa ripoti ya uhalifu wa ngono kwa polisi.

Papa Francis mnamo siku ya Ijumaa 29/03/19 pia alitoa miongozo ya ulinzi wa watoto na katika seminari zake za vijana kwenye mji wa Vatican. Hatua hiyo ni baada ya kashfa ya unyanyasaji wa kingono duniani kulipuka tena upya mnamo mwaka jana na pia baada ya shirika la habari la Associated Press kuripoti kwamba makao makuu ya Kanisa Katoliki hayakuwa na sera ya kuwalinda watoto kutoka kwa mapadri wenye roho za kinyama.

 Mwana Seminari wa zamani Kamil Jarzembowski  amesema hatua hiyo ni muhimu na pia ni mfano mzuri na ya kutia moyo japo kanuni hiyo mpya kwanza itafanya kazi kwenye jimbo la Vatican City, kwenye taasisi zake na katika ngazi ya kidiplomasia. Madhila yaliyompata Jarzembowski yamechangia pakubwa kuleta mageuzi hayo. Kamil Jarzembowski aliliambia shirika la habari la AP kwamba hii ni hatua nzuri.

Sheria hii kwa mara ya kwanza inatoa ufafanuzi wa wazi ambao watu wazima wana haki ya kulindwa sawa na watoto kwa mujibu wa sheria za Kanisa. Vatican katika miaka kadhaa iliyopita, ilirekebisha sheria yake na kuongezea kifungu kuhusu unyanyasaji wa kingono na kuwahusisha watu wazima walio katika mazingira magumu lakini ilikuwa haikufafanua.

Kwa mujibu wa ufafanuzi mpya wa Vatican, mtu aliye kwenye mazingira magumu ni mtu ambaye ni mgonjwa au anayesumbuliwa na athari zozote kimwili au kiakili, mtu mwenye ufahamu mdogo na ambaye hawezi kuutumia uhuru wa kibinafsi, na pia mtu mwenye uwezo mdogo wa kuelewa au kupinga kitendo cha uhalifu.

Watawa walio watu wazima wakiwemo Masista ambao huwategemea viongozi wa Kanisa kihisia au kifedha wanaweza pia kuchukuliwa kuwa ni watu walio katika mazingira magumu kwa kuuzingatia kama mfano kashfa ya Kardinali Theodore McCarrick wa Marekani, aliyekabiliwa na shutuma za kuwadhalilisha watawa. Vilevile taarifa kuhusu mapadri na maaskofu waliowadhulumu kingono watawa.

Sheria hiyo mpya inawahusu wafanyakazi wote wanaoishi na kufanya kazi katika Vatican, mji mkuu wa Kanisa Katoliki wenye ukubwa wa ekari 110 katikati ya mji wa Roma, pia katika balozi zinazoliwakilisha Kanisa Katoliki kote ulimwenguni.

Sheria mpya inasisitiza kuwapokea waathirika, kuwasikiliza na kuhakikisha kwamba wanapewa msaada wa matibabu, kisaikolojia na kisheria. Waathirika na familia zao watalindwa na matendo yoyote ya kulipizwa kisasi, na pia kutafuta majibu ya matatizo ya muda mrefu yanayowakabili watu walioathirika na vitendo vya unanyasaji.

Chanzo/APE