1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Kanisa lijiokoe lenyewe"

Maja Dreyer11 Juni 2007

Katika siku tano zilizopita Wakristo wa Ujerumani wa madhehebu ya Kiprotestanti walikusanyika mjini Cologne. Zaidi ya waumini millioni mmoja walishiriki kwenye hadhara hiyo inayofanyika kila mwaka. Kuna baadhi ya wahariri ambao wanasema kanisa la Kiprotestani limeshindwa kupandisha sauti juu ya masuala ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/CHSk
Kwenye misa ya mwisho ya Siku ya Kanisa
Kwenye misa ya mwisho ya Siku ya KanisaPicha: AP

Gazeti la “Berliner Morgenpost” lakini lina maoni mengine:

“Siku ya kanisa ambayo kwa muda mrefu ilitumika kama mahala pa mjadala wa kisiasa, bado ilijihusisha na masuala ya siasa – kinyume cha malalamiko yaliyotolewa. Kwa kweli, washirika walijiingiza kwa nguvu katika mjadala juu ya utandawazi na mkutano wa viongozi wa nchi za kundi la G8. Pia kanisa limechukua msimamo wazi kuhusiana na Uislamu, yaani kwamba katika masuala ya uhuru wa dini, uhuru wa kubadilisha dini na usawa kati ya wanaume na wanawake kanisa hili halitakubali haki hizo zikandamizwe.”

Naam, mkutano huu uligusa sana mahusiano kati ya madhehebu mbali mbali. Mhariri wa “Märkische Oderzeitung” lakini anatoa mwito kwa Wakristo kujishughulisha pia na matatizo ya ndani. Ameandika:

“Ni sawa kwamba kanisa linapaswa kutoa muongozo wa maadili. Lakini wakati linapojaribu kujenga madaraja na madhehebu nyingine lisisahau kuwa linashindwa kuimarisha jamii ya waumini. Tungependa sana kujua zaidi vipi kanisa hili linataka kupambana na idadi kubwa na watu wanaojiunga na makundi ya kiinjili au vikundi vingine. Dunia inaweza kuokolewa na wengi, lakini kanisa la Kiprotestani lazima lijiokoe lenyewe.”

Juu ya jukumu la makanisa katika jamii yetu, mhariri wa gazeti la “Münchner Merkur” ana haya ya kusema:

“Wakati umefika kuwa madhehebu mawili makubwa ya Kikristo yajitolee zaidi kuzungumza na upande wa siasa na kurekebisha sera za kijamii. Wasiwasi juu ya watu maskini na kulinda uumbaji wa Mungu ni masuala muhimu Wakristo wanapaswa kuyashughulikia na kurudi kwenye jukwaa la kisiasa. Ila tu mwito wa mwenyekiti wa mkutano wa Cologne kudai wanasiasa wakae pamoja na kuzungumza na Wataliban na magaidi haufai hata kidogo.”

Suala la pili linalozingatiwa na wahariri wa magazeti ya hapa nchini ni uchaguzi wa bunge nchini Ufaransa ambapo kama tulivyosikia katika ripoti zetu, chama cha kihafidhina cha rais mpya Nikolas Sarkozy kilishinda kwa wingi mkubwa. Matokeo haya yana maana gani? Haya hapa maoni ya “Nordwest-Zeitung”:

“Wafaransa wanakubaliana kuwa wanataka kuanza upya kabisa. Tena mwanzo huo mpya una jina moja: Nikolas Sarkozy. Baada ya chama chake kushinda katika duru hiyo ya kwanza ya uchaguzi, kinatarajiwa kushinda pia katika duru ya pili Jumapili ijayo. Hivyo, rais Sarkozy na mrengo mzima wa kihafidhina utakuwa na mamlaka makubwa, na Sarkozy anaweza kutekeleza mageuzi kama anavyopenda.”

Ni maneno yake mhariri wa “Nordwest-Zeitung”. Hatimaye tunalinukuu gazeti la hapa mjini Bonn, “Generalanzeiger”, ambalo limeandika yafuatayo:

“Baada ya chaguzi hizo kuu za Ufaransa, Sarkozy amehakikishiwa kwa njia mbili atekeleze mageuzi aliyoyaahidi. Baada ya kushinda chama chake, hatakabiliwa na upinzani kutoka bungeni. Ndio maana, lakini, upinzani utaonekana mabarabarani kupitia maandamano, kama kawaida, wakati matokeo ya kwanza ya mageuzi yataonekana.”