1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela akutana na mkuu wa Benki kuu ya Ulaya

26 Septemba 2012

Kansela Angela Merkel alikutana leo (25.09.2012) mjini Berlin na mkuu wa Benki Kuu ya Ulaya, Mario Draghi.Ilitajwa kwamba watu hao walibadilishana, mawazo juu ya masuala ya uchumi na Umoja wa Sarafu ya Ulaya.

https://p.dw.com/p/16Ecj
Mkuu wa Benki Kuu ya Ulaya Mario Draghi
Mkuu wa Benki Kuu ya Ulaya Mario DraghiPicha: AP

Kiini cha mazungumzo hayo ni lile tangazo la Mario Draghi kwamba Benki Kuu ya Ualya, ikiwa ni dharura, itanunua dhamana za mikopo kutoka nchi za eneo la sarafu ya Euro ambazo ziko katika mzozo wa kifedha. Jambo hilo limekataliwa hasa na rais wa Benki Kuu ya Ujerumani, Jens Weidmann. Pia lawama juu ya mpango huo zimetolewa miongoni mwa wanasiasa wa serikali ya mseto ya Ujerumani.

Akihutubia mkutano mkuu wa Shirikisho la wanaviwanda wa Ujerumani hii leo (25.09.2012), Kansela Angela Merkel alizionya nchi za eneo la sarafu ya Euro zisikimbilie moja kwa moja kuwa na muungano wa mabenki, huku kukiweko ishara kwamba Ujerumani imeingiwa na wasiwasi mpya kuhusu hali ya uchumi katika Ugiriki na Uhispania. Aliyakataa matakwa, hasa yanayotolewa na komisheni ya Umoja wa Ulaya na Ufaransa, kwamba kuundwe kwa upesi kama iwezekanavyo chombo cha Umoja wa Ulaya cha kuyasimamia mabenki, chombo ambacho baadae kitayasaidia mabenki yalio mashakani. Alisema yeye anaunga mkono usimamizi mkali zaidi wa mabenki katika eneo la sarafu ya Euro, lakini usimamizi huo lazima zaidi uwe wa lazima, kwani yeye hawezi kuzungumzia juu ya kutoa mitaji mipya kwa mabenki katika nchi nyingine, ikiwa hakutakuweko ile haki ya kuingilia kati. Alisema msimamo uwe ni kwenda hatua kwa hatua na kwa njia sahihi, na sio kwa pupa, sio tu kuweza kusema sasa tuna kitu.

Ujerumani inaona hatua za tahadhari ni muhimu zaidi

Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya walikubaliana mwezi Juni kwamba fedha za uokozi za Umoja huo zinaweza kutumiwa moja kwa moja kuyapa mitaji mabenki yalio katika shida, lakini tu pale kitakapoundwa chombo cha usimamizi Ulaya kote, chini ya uongozi wa Benki Kuu ya Ulaya. Lakini kuna ufa mpya unaoonekana katika Umoja wa Ulaya. Ujerumani inaona hatua za tahadhari ni muhimu zaidi kuliko zile za haraka, ambapo Rais Francois Hollande wa Ufaransa alisema mwishoni mwa wiki iliopita kwamba kila mpango huo utakapoanzishwa mapema ndivyo itakavokuwa bora.

Matamshi hayo ya Bibi Merkel yamekuja kukiweko na ushahidi kwamba uchumi wa Ujerumani, ulio mkubwa kabisa barani Ulaya, unazidi kuathirika na mzozo wa sarafu katika Ulaya, na akatahadharisha kwamba hata Ujerumani haitaweza daima kuyaepuka maumivu hayo.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters

Imani ya wateja hapa Ujerumani inapungua. Kwa hivyo, Kansela Merkel alionya kwamba Ujerumani sio kisiwa, lakini kama nchi ilio na nguvu katika kuuza ng'ambo bidhaa zake haiwezi kuepuka na hali ya mambo inavoendelea duniani na katika uchumi wa nchi za Ulaya. Alisema wao wana jukumu kufanya kila kinachowezekana kwa ajilli ya mahitaji ya wateja wa ndani hapa Ujerumani ili waupige jeki uchumi wa nchi za Sarafu ya Euro.

Wakati huo mnada wa dhamana za mikopo huko Uhispania na Italy haujatoa matumaini makubwa, kwa vile gharama za kukopa katika nchi hizo zimepanda.

Pia wanasheria wa Benki Kuu ya Ulaya wanachunguza uhalali wa huo mpango uliotangazwa na benki hiyo wa kununua dhamana za mikopo ya nchi zilizo taabani kifedha ndani ya eneo la sarafu ya Euro. Mikataba ya Umoja wa Ulaya inaikataza benki hiyo kuzikopesha moja kwa moja serikali, lakini benki hiyo inaruhusiwa kununua dhamana za mikopo. Kuna wasiwasi kwamba wabishi wa mpango huo wanaweza kulieleka suala hilo liamuliwe na mahakama kuu ya Ulaya.

Mwandishi: Miraji Othman/dpa/afpa

Mhariri: Mohammed Abdulrahman