1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Angela Merkel aelekea Marekani

Oumilkher Hamidou2 Novemba 2009

Ziara ya kwanza ya kansela Merkel nchini Marekani baada ya kuchaguliwa upya kuiongoza Ujerumani kwa kipindi chengine cha miaka minne

https://p.dw.com/p/KLhg
Barack Obama aliamini tangu mwanzo Angele Merkel ataibuka na ushindiPicha: dpa

Hata kabla ya kuhutubia bunge la shirikisho kufafanua sera za serikali yake,kansela aliyechaguliwa upya hivi karibuni Angela Merkel anaondoka Berlin leo hii kuelekea Washington.Kesho jumanne kansela Angela Merkel atayahutubia mabaraza yote mawili ya Congress ya Marekani:Hii ni hishma kubwa kwa mwanasiasa huyo wa chama cha Christian Democratic na inamaanisha umuhimu wa Ujerumani kwa Marekani.Lakini hishma hiyo si ya bure.Marekani inategemea badala yake kuiona serekali mpya ya Ujerumani ikiwajibika zaidi katika siasa ya nje.

Kwanza ni kuhusu kuwepo vikosi vya jeshi la shirikisho Bundeswehr nchini Afghanistan.Ingawa Ujerumani inashikilia nafasi ya tatu ya nchi zilizotuma wanajeshi kutumikia juhudi za kulinda amani za NATO nchini Afghanistan,lakini shughuli za wanajeshi hao 4400 zimewekewa vikomo na bunge la shirikisho Bundestag.Wanaruhusiwa kujihami,lakini sio kushambulia,na madege ya kivita ya Bundeswehr-Tornados,ingawa yanasaidia katika kufanya upelelezi wa angani,lakini hazisaidii katika mapigano.

Kabla ya rais Obama kuitaka rasmi Ujerumani na mataifa mengine shirika yafanye chochote kile,atalazimika kwanza kuamua juu ya mustakbal wa Afghanistan.Ni dhahiri kwamba serikali ya Marekani ingependelea kuiona Ujerumani ikiwajibika zaidi nchini Afghanistan.Rais Barack Obama kila wakati amekua akisisitiza kwamba Marekani haitoweza peke yake kudhamini ujenzi mpya wa Afghhanistan,na kupambana na wafuasi wa Al Qaida na Taliban.

Mada ya pili inayotazamiwa kujadiliwa ni kuhusu wafungwa wa Guantanamo.Marekani ingependelea sana kuiona Ujerumani ikikubali kuwapokea wafungwa japo kidogo wa Guantanamo ambao hawawezi kurejeshwa makwao kwa hofu wasije wakaadhibiwa.

Hata katika suala la uhusiano mpya kati ya Marekani na Urusi,Ujerumani inashikilia nafasi muhimu.Ushirikiano wa dhati wa kiuchumi kati ya Ujerumani na Urusi hauangaliwi kwa jicho jema nchini Marekani.Mshauri wa masuala ya usalama wa rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter,ameonya Urusi isije ikajipatia maridhiano makubwa ya kisiasa kwa masilahi ya kiuchumi.

Hata katika uhusiano wa Marekani pamoja na Iran,Ujerumani inashikilia nafasi muhimu kutokana na uhusiano wake wa kiuchumi pamoja na nchi hiyo.Biashara ya Ujerumani kwa Iran,licha ya kupungua,inafikia mabilioni ya yuro kwa mwaka.Zaidi ya hayo Ujerumani,pamoja na mataifa matano wanachama wa kudumu wa baraza la usalama,inashiriki katika mazungumzo ya mradi wa kinuklea wa Iran.Katika suala la vikwazo dhidi ya Iran,Marekani ingependelea kuiona Ujerumani ikiiwekea Teheran vikwazo hasa,pindi vikitangazwa na Umoja wa mataifa,badala ya kuunga mkono.

Mada zote hizo zinaifungulia njia Ujerumani kusimama upande wa Marekani.Stephen Szabo -mkurugenzi wa taasisi ya Ujerumani ya Marschall Fund mjini Washington anasema:

"Wajerumani wanabidi watambue kwamba marekani imebadilika.Marekani hii nmpya inapitisha maamuzi yake kwa uangalifu zaidi na haijibebeshi majukumu makubwa kama zamani.Ndio maana inahitaki washirika madhubuti barani Ulaya ili kukabidliana na matatizo yaliyopo.

Kwa mujibu wa mtaalam huyo wa masuala ya kisiasa,Ujerumani isipoteze muda mrefu kujitokeza kama mshirika madhubuti.Kwasababu wamarekani hawana subira.

Mwandishi:Christina Bergmann/ZR/Oummilkheir Hamidou

Mhariri:M.Abdul-Rahman

: