1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel atoa tamko la serikali

Abdu Said Mtullya18 Oktoba 2012

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema sarafu ya Euro siyo fedha tu bali pia ni msingi wa Umoja wa Ulaya kiuchumi, kisiasa na kijamii na amependekeza njia mpya katika kupambana na mgogoro wa madeni.

https://p.dw.com/p/16Rt3
Bundeskanzlerin Angela Merkel (CDU) gibt am 18.10.2012 im Bundestag in Berlin eine Regierungserklärung ab. Foto: Wolfgang Kumm/dpa +++(c) dpa - Bildfunk+++
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa

Kansela Merkel ameyasema hayo muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya mjini Brussels. Akizungumza Bungeni mjini Berlin, kutoa tamko la serikali, Kansela Merkel pia ametoa mwito wa kuleta ustawi zaidi. Akisisitiza umuhimu wa sarafu ya Euro, Kansela wa Ujerumani amesema kuwa "Sarafu ya Euro, siyo fedha tu." Amesema Euro ni ishara hai ya umoja wa Ulaya kisiasa, kiuchumi na kijamii na kwamba ina uzito pia nje ya bara la Ulaya.

Katika tamko la serikali alilolitoa bungeni, Kansela Merkel pia amesifu juhudi zilizofanyika hadi sasa katika kukabiliana na mgogoro wa Euro na ametoa mwito wa kuanzisha mifuko mipya ili kuzisaidia serikali zilizolemewa na madeni ili ziweze kufadhili miradi maalamu. Ameeleza kuwa kwa njia hiyo itawezakana kuanzisha kigezo kipya cha mshikamano katika juhudi za kupambana na mgogoro wa madeni.

Merkel aunga mkono pendekezo

Katika tamko lake Kansela Merkel pia ameunga mkono pendekezo la kuipa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya mamlaka juu ya bajeti za nchi wanachama za Umoja wa sarafu ya Euro. Bibi Merkel pia amesema juhudi za kuukabili mgogoro wa Euro zitaaendelea kufanywa hata baada ya mkutano wa mjini Brussels. Amesema mikutano mingine itafuatia.

Kansela Merkel amesema anapendelea sana kuona kwamba Ugiriki inaendelea kuwamo katika Umoja wa sarafu ya Euro kwa sababu amesema, pamoja na kuwa rafiki na mshirika wa jumuiya ya kujihami ya NATO, Ugiriki ni sehemu ya Ulaya. Lakini bibi Merkel ameshutumu rushwa nchini Ugiriki. Kiongozi huyo wa Ujerumani kwa mara nyingine amepinga wazo la kuyaleta pamoja madeni ya nchi zote ili yalipwe na nchi zote.

Peer Steinbrueck, German social democratic party SPD deputy and candidate for the position of federal chancellor in next year's election, addresses the Bundestag (lower house of parliament) in Berlin on October 18, 2012 after German Chancellor gave a speech. Merkel earlier outlined Germany's position ahead of a summit of European Union leaders in Brussels. AFP PHOTO / JOHANNES EISELE (Photo credit should read JOHANNES EISELE/AFP/Getty Images)
Peer Steinbrück mgombea ukanselaPicha: AFP/Getty Images

Akizunguma kujibu tamko la serikali mjumbe atakayegombea ukansela kwa tiketi ya chama kikuu cha upinzani, SPD, Bwana Peer Steinbrück, amemlaumu Kansela Merkel kwa undumakuwili katika juhudi za kupambana na mgogoro wa madeni. Amemtaka Kansela Merkel aseme kwamba, kuhusu Ugiriki, Ujerumani inapaswa kutimiza wajibu zaidi kwa kushirikiana na nchi nyingine.

Mkutano wa kilele wa viongozi kutoka nchi 27 za Umoja wa Ulaya mjini Brussels utajadili mustakabali wa sarafu ya Euro na njia za kuondokana na mgogoro wa madeni.

Mwandishi: Mtullya Abdu/dpae, ZA

Mhariri: Josephat Charo