1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel 'avunjwa moyo' na hatua ya Trump kuhusu G7

Daniel Gakuba
11 Juni 2018

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amemkosoa vikali Rais Donald Trump wa Marekani, kwa hatua yake ya kukataa kuidhinisha azimio la mkutano wa kilele wa kundi la G7. Bi Merkel amesema ''Ulaya haitaendelea kudhulumiwa''.

https://p.dw.com/p/2zFkL
Deutschland Bundeskanzlerin Angela Merkel zu Gast bei Anne Will
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika mahojiano na kituo cha ARDPicha: picture-alliance/dpa/NDR/W. Borrs

Bi Angela Merkel ameyaeleza maoni yake kupitia mahojiano na kituo cha televisheni cha ARD, baada ya kuwasili nchini Ujerumani kutoka mkutano wa kilele wa kundi la nchi zilizoendelea kiviwanda, G7 uliofanyika nchini Canada mwishoni mwa juma lililopita. Merkel amesema hatua ya Rais Trump kuondoa saini yake kwenye tangazo la mwisho wa mkutano huo wa viongozi wa nchi, ilikuwa ni ya kuwazindua watu waelewe hali halisi, na pia ya kuvunja moyo.

Trump ambaye alikuwa kiongozi wa mwisho kuwasili katika mkutano huo na wa kwanza kuondoka, alitangaza kupitia mtandao wa twitter kwamba amewaamuru maafisa wake kubatilisha uamuzi wa awali wa kuunga mkono tangazo la mwisho la mkutano huo.

''Umoja wa Ulaya utasonga mbele kutangaza hatua za kulipa kisasi dhidi ya uamuzi wa Rais Trump kuziwekea adhabu ya nyongeza ya ushuru kwa bidhaa za chuma na bati, kwa sababu hatuwezi kuruhusu kuendelea kudhulumiwa.'' Amesema Bi Merkel kwa ukali ambao sio kawaida yake.

Hatua za kulipiza kisasi

Umoja wa Ulaya, na pia Canada ambayo pia imewekewa ongezeko la ushuru, zinatarajia kutangaza hatua hizo za kisasi dhidi ya Marekani ifikapo Julai 1.

G7 Gipfel Kanada Gruppenbild
Tangu mwanzoni mkutano wa G7 nchini Canada ulighubikwa na kiwingu cha uhasama wa TrumpPicha: Reuters/L. Mills

Rais Donald Trump alisababisha mvutano mkubwa kwa ujumbe alioutuma kupitia mtandaom wa twitter mara tu baada ya kuondoka Canada, akimshambulia waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau, aliyemuita mtu 'mnyonge na asiye mwaminifu'.

Alipoulizwa kwa nini aliendelea kuonekana mtulivu wakati sakati hilo likiendelea, Kansela Merkel alijibu kuwa kuendeleza vita vya maneno hakuwezi kuwa na tija yoyote.

Merkel alisema aliarifiwa kuhusu uamuzi wa Trump akiwa safarini kurejea nyumbani, akisema kilichotokea 'kinafumbua macho na kuvunja moyo'.

Juhudi za ushirikiano kuendelea

Kanada Staats- und Regierungschefs G7-Staaten diskutieren gemeinsame Erklärung in Charlevoix
Trump alionekana kutengwa na viongozi wenzakePicha: Reuters/Prime Minister's Office/A. Scotti

Hata hivyo, licha ya hatua hiyo ya Marekani kutupilia mbali azimio la mkutano wa G7 na kushikilia msimamo wa kuziwekea bidhaa za nchi washirika zinazoingia kwenye soko la Marekani, Kansela Merkel amesema ataendelea kufanya kazi na Rais Trump.

''Bado kuna sababu muhimu ya kuendelea kupigania uhusiano mwema kati ya Marekani na Ulaya'', amesema Bi Merkel na kuongeza kuwa vita vya kibiashara baina ya pande hizo haviwezi kuweka kikomi kenye ushirikiano uliopo.

Rais Trump na Kansela Merkel wanatarajiwa kukutana tena katika mkutano wa kilele wa nchi wanachama wa Umoja wa Kujihami wa NATO, ambao utafanyika mjini Brussels mwezi ujao wa Julai.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, afpe

Mhariri: Iddi Ssessanga